Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kujipanga kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali ili kudhibiti vifo vinavyotokana na ajali pamoja na makosa ya barabarani. Rais Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo tarehe 6 Januari, 2026 alipokutana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa George Simbachawene, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo ya kikazi.

Amesema kukamilika kwa mfumo huo wa kidigitali pamoja na matumizi ya taa za usalama barabarani (Traffic Lights) na uwekaji wa rada za kudhibiti kasi, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti makosa yanayofanyika barabarani, kupunguza vifo vinavyotokana na ajali pamoja na kupunguza gharama za huduma za afya zinazobebwa na Serikali baada ya ajali kutokea.

Akizungumzia suala la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, ikiwemo vitendo vya ubakaji, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imechukua hatua madhubuti kudhibiti vitendo hivyo, ikiwemo kuondoa dhamana kwa watuhumiwa wa makosa hayo, pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma dhidi ya udhalilishaji.

Halikadhalika, akizungumzia matukio ya uhalifu na makosa katika maeneo ya utalii, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuchukua juhudi kubwa za kuimarisha usalama katika maeneo hayo, ikiwemo kuwataka wamiliki wa hoteli kuweka kamera za CCTV ili kusaidia kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Rais Dkt. Mwinyi amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hususan katika kuimarisha utendaji wa pamoja wa sekta za Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Jeshi la Polisi, na kusisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe.George Simbachawene, ameonesha kuridhishwa na mchango na ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha utendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, ikiwemo Uhamiaji, NIDA na Polisi.