SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuwalipa fidia ya vipando na majengo wananchi wote wa eneo la Bumbwini waliopitiwa na mradi wa barabara na ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na wananchi wa Bumbwini Misufini, shehia ya Kidanzini, kijiji cha Mwembe mdema, Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa nyumba za fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo kijijini hapo.

Amesema, tayari zoezi la ulipwaji wa fidia kwa baadhi ya wananchi hao limeanza kwa wakaazi wa Mangapwani na baadae kumalizia vijiji nyengine vilivyopitiwa na miradi hiyo.“Kwa wale wote wanaostahili kulipwa fidia iwe ya vipando au majengo, tunahakikisha fidia zenu mtalipwa nyote kwa kipidi kifupi” Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi hao.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwashauri viongozi wa jimbo hilo, kushirikiana na Mkandarasi wa mradi wa nyumba za wananchi zinazoendelea kujengwa kwenye maeneo ya Mwembe mdema, Shehia ya Kidanzini na nyumba za Mangapwani kwa kuangalia mahitaji halisi ya aina ya nyumba wananchi watakazoridhika nazo.Pia, aliishauri kamati inayosimamia ujenzi wa nyumba hizo, kushirikiana na mkandarasi kujenga nyumba zitakazokidhi haja za walengwa ili kuwaepushia usumbufu wa baadae.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Dk. Khalid Salum Muhamed, amesema hatua za ujenzi wa awali wa nyumba hizo zitasaidisha kuboshesha mwendelezo wa nyumba zitakazofuata kwa kuepuka changamoto zilizojitokeza baada ya kukamilika nyumba mbili za mwanzo.Akigusua suala la fidia Dk. Khalid pia alieleza mbali ya fidia za mazao na nyumba lakini wananchi waliopoteza maeneo yao, ikiwemo viwanja alisema, tayari Serikali imeunda kamati inayojumuisha wataalamu wa ardhi na wanasheria kulishighulikia suala hilo ili kukamilisha ahadi ya Serikali ya kulipwa na kueleza tayari eneo hilo limefanyiwa tathmini na tayari ripoti imetoka.

Nae, Mkandarasi wa ujenzi wa nyumba hizo kampuni ya “Orkun” kutoka Uturuki, imeiahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya maboresho kwa mujibu ya maelekezo wanayokubaliana.Ujenzi wa nyumba hizo unatarajiwa kukamilisha nyumba 370 kwa wananchi wa maeneo ya Bumbwini Misufini pamoja na wakaazi wa maeneo ya Mangapwani ikiwa ni sehemu ya fidia yao watakayopewa na Serikali baada ya kupisha miradi ya maendeleo iliwemo miundombinu ya barabara na ujenzi wa bandari kubwa ya Mangapwani.

Ujenzi huo pia utahusisha maduka ya biasahara na skuli ya maandalizi, miundombinu ya maji safi na maji taka, zikiwemo barabara za ndani ya eneo hilo za kiwango cha lami pamoja na mitaro ya maji machafu.