Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itaendelea kuimarisha Ushirikiano wa kiuchumi na Diplomasia na Msumbiji kwa manufaa ya Nchi hizo mbili.Dkt,Mwinyi ameeleza hayo alipokuwa na Mazungumzo na Rais wa Msumbiji Daniel Francisco Chapo ambaye yupo nchini kwa ziara maalum yaliofanyika Ikulu.
Dk Mwinyi amesema ziara hiyo itachochea kuimarisha Udugu na Umoja wa muda Mrefu uliopo baina ya nchi hizo rafiki.Ameeleza kuwa Uamuzi wa kufanya ziara ya Kwanza Tanzania ikiwemo Zanzibar baada ya Kuchaguliwa kunaonesha Kuthamini Ushirikiano huo ulioasisiwa na Viongozi Waasisi wa Mataifa hayo.
Akizungumzia Masuala ya Kiuchumi Dkt, Mwinyi amesema yapo maeneo mengi na fursa za Ushirikiano ambayo nchi hizo zinaweza kubadilishana Uzoefu katika nyanja mbalimbali sambamba na Ushirikiano wa kidiplomasia.Rais Dkt, Mwinyi amebainisha Maeneo Matano ya kiuchumi ambayo nchi hizo zinaweza kushirikiana kuwa ni Uchumi wa Buluu, Mafuta na Gesi, Uvuvi wa Bahari Kuu, Utalii na Uwekezaji .
Ameeleza kuwa Uzoefu wa Msumbiji katika sekta ya Mafuta na Gesi ni eneo muhimu la Kiuchumi ambalo Zanzibar inaweza kujifunza kupitia Uzoefu huo wa takribani miaka 20 wa Msumbiji katika sekta hiyo. Rais Dkt,Mwinyi ameeleza kuwa Mafanikio ya Zanzibar katika Sekta ya Uchumi wa Buluu nayo ni Sekta Muhimu ambayo Msumbiji inaweza kujifunza kutokana na Mafanikio ya sekta hiyo hapa nchini.
Akizungumzia Utalii amesema zipo fursa nyingi zinazopaswa kuwekewa Mkazo na Mataifa hayo pamoja na Mafanikio ya Zanzibar katika eneo hilo ambalo linachangia asilimia 30 ya mapato ya nchi.Akizungumzia Lugha ya Kiswahili Dkt, Mwinyi amesema ni fursa nyengine muhimu ya Ushirikiano itakayowezesha nchi hizo kubadilishana Walimu kwa Zanzibar kutoa Walimu wa Kiswahili na Msumbiji kutoa Walimu wa Lugha ya Kireno kujifunza hatua ikayochangia kuchochea Utalii kwa nchi hizo .
Aidha Rais Dkt,Mwinyi ameihakikishia Msumbiji kuwa Serikali itaendelea kutoa Ushirikiano wa kutosha kwa Wananchi wenye asili ya Msumbiji Waliopo Zanzibar wanaofikia 3000 ambao tayari wengine wameshapewa Uraia wa Tanzania.Rais Dkt, Mwinyi amempongeza Rais Chapo kwa Ushindi alioupata katika Uchaguzi wa Mkuu wa nchi hiyo aliouelezea kuwa Unazidisha Ushirikiano na Umoja Uliopo baina ya Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Frelimo.
Naye Rais Daniel Fransisco Chapo amesema Msumbiji ina dhamira ya dhati ya Kuimarisha Ushirikiano na Zanzibar na ziara yake imelenga kukamilisha azma. hiyo.Rais Chapo ameeleza kuwa ziara hiyo itafungua milango na fursa za Kiuchumi baina ya nchi hizo pamoja Uhusiamo wa kidiplomasia wa muda mrefu.
Ameipongeza Zanzibar kwa mafanikio inayoyapata kupitia Sekta ya Utalii na Uchumi wa Buluu na kwamba Msumbiji ina kila sababu ya Kujifunza.Alizungumzia Sekta ya Mafuta na Gesi amesema Msumbiji imepiga hatua kubwa katika Maendeleo ya Sekta hiyo na kuihakikishia Zanzibar kuwa Nchi yake ipo tayari kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo kwa Kuwa na mazungumzo na timu za Watendaji wa pande zote mbili.