Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Benki ya Stanbic Tanzania wa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa mikakati na mipango ya maendeleo iliyopangwa.Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya Stanbic Tanzania, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake Kevin Wingfield.
Katika mazungumzo hayo Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa azma ya Benki ya Stanbic ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasaidia kwa kiasi kikubwa hasa kwa vile Beki hiyo ina mpango wa kuanzisha Tawi lake hapa Zanzibar.Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi wa Benki hiyo mikakati ya maendeleo iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Sera yake ya Uchumi wa Buluu, sekta za kijamii na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Rais Dk. Mwinyi alieleza fursa zilizopo katika uchumi wa Buluu na kusisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Benki hiyo katika Sera yake ya Uchumi wa buluu hasa katika vipaumbele vyake ilivyoviweka.Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alivitaja miongoni mwa vipaumbele hivyo vilivyomo katika uchumi wa buluu kuwa ni sekta ya utalii, uvuvi wa Bahari kuu, mafuta na gesi asilia, bandari, usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wa sekta ya uvuvi Rais Dk. Mwinyi alieleza namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyokusudia kuwakomboa wavuvi kwa kuwapa utaalamu pamoja na nyenzo za kisasa hasa wavuvi wadogo ambao kwa muda mrefu kipato chao kilikuwa ni kidogo ikilinganishwa na shughuli wanazozifanya.Mbali ya mikakati iliyowekwa na Serikali katika uchumi wake kupitia Sera ya uchumi wa buluu, Rais Dk. Mwinyi uliueleza uongozi huo jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta kadhaa za maendeleo na kuwakaribisha wawekezaji kupitia benki hiyo kuja kuekeza Zanzibar.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Kevin Wingfield alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya Benki hiyo kufungua Tawi lake hapa Zanzibar hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujiletea maendeleo.Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kueleza uzoefu, mikakati pamoja na shughuli za benki hiyo hasa katika kuunga mkono harakati za maendeleo katika sekta ya umaa na sekta binafsi ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ikizingatiwa kwamba benki hiyo ina matawi yake katika nchi mbali mbali duniani.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alifanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Italia ambao wameonesha nia ya kuja kuekeza Zanzibar kutokana na mazingira mazuri yaliyopo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono sera ya uchumi wa buluu.