Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Seychelles Mheshimiwa Danny Faure katika ukumbi wa Hoteli ya Intercontinental Mjini Nairobi Leo na kueleza kwamba Zanzibar na Seychelles zina mazingira ya kijiografia na shughuli za kiuchumi zilizofanana na watu wa nchi hizo wamekuwa wakishirikiana katika shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Katika mazungumo hayo, Dk Shein alihimiza haja ya kuimarisha uhusiano wa kidugu na kihistoria uliopo baina ya nchi mbili hizo. Katika kikao hicho Dk. Shein alikumbushia mambo mbali mbali waliozungumza na Rais wa Zamani wa Seychelles Mheshiwa James Michel walipokutana wakati wa Mkutano wa Nchi za Visiwa wa Samoa mwezi Septemba mwaka 2014.
Alisema viongozi hao walipokutana walizungumza haja ya kuimarisha mashirikiano katika masuala mbali mbali ya uchumi wa bahari, ikiwemo sekta ya utalii, uvuvi , usafiri wa anga na masuala, kwa kuzingatia kwamba hayo ni maeneo muhimu ya kiuchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA).
Dk. Shein alisema kwamba itakuwa ni vyema Serikali iliyopo madarakani hivi sasa na Rais Danny Faure ni vyema ikaendeza ushirikiano katika maeneo hayo na mengine mapya kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na mwenendo wa kiuchumi wa hivi sasa.
Aidha, Dk Shein alileleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaendeleza kushirikiana na Serikali ya Seychelles katika masuala ya ulinzi na salama.
Vile vile, alihimiza haja ya viongozi wa pande hizo mbili kuwa na utaratibu wa kutembeleana mara kwa mara,na kusisitiza haja ya viongozi pia kukutana pamoja kwa ajili ya kubainisha na hatimae kutiliana saini maeneo ya ushirikiano baina ya Seychelles na Zanzibar .
Kwa upande wake Mheshimiwa Danny Faure alitoa shukurani kwa Dk . Shein kwa kutenga muda maalumu wa kukutana kwa ajili ya kujadili masuala muhimu ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa pande mbili hizo.
Alieleza kwamba ushirikiano biana ya Seychelles na Zanzibar una historia refu na umezidi kuimairika baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alitoa historia ya ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Seychelles kabla ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1976 na baada ya kupata huru.
Alieleza kwamba wananchi wa Seychelles wanakumbuka na kuthamini mchango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala mbali mbali ya kiuchumi, kiulinzi na kiusalama, na watahakisha wanaendeleza uhusiano huo.
Alieleza kwamba amefurahi kupata taarifa ya mazungumzo aliyofanya Dk. Shein na Seychelles na Rais aliyeondoka madarakani, James Michel walipokutana wakati wa Mkutano wa Nchi za Visiwa wa Samoa mwezi Septemba mwaka 2014.
Alisema kwamba maeneo ya ushiriakiano waliyohadili nchini Samoa ni muhimu na Serikali yake iko tayari kuyaendeleza na kuongeza maeneo mapya ambayo yataonekana muhimu kwa pande mbili hizo.
Alieleza kwamba nchi yake iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii, biashara, uhifadhi wa mazingira, ulinzi na usalama na maeneo yote muhimu katika kuendeleza uchumi endelevu wa bahari kama kwa kuzingatia malengo ya mkutano wa uchumi endelevu wa bahari uliowakutanisha viongoi hao mjini Nairobi
Mheshimiwa Danny Faure nae alisititiza juu ya haja ya viongozi wakuu wa sekta mbali mbali wa Zanzibar na Seychelles kukutana kwa ajili ya kujadili na hatimae kusaini makubalino ya maeneo ya ushirikiano kwa faida ya pande zote mbili.
Viongozi hao waliagana kwa kila mmoja kumtakia mwenzake safari njema ya kurudi nyumbani.