RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa wanawake wa Tanzania ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Tanzania Bara na Zanzibar hivyo ni vyema wakapewa kipaumbele ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, ulioongozwa na Mwenyekiti wa Umoja huo Gaudensia Kabaka ambao ulifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, aliueleza uongozi huo kuwa wanawake wana nafasi maalum katika Chama na Serikali kutokana na majukumu yao sambamba na juhudi zao.

Rais Dk. Shein alisema kuwa bila ya akina mama mafanikio zaidi hayatofikiwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndani ya (CCM) hasa ikizingatiwa kuwa wana umuhimu mkubwa katika jamii.

Alieleza kuwa kina mama ni vyema wakapewa nafasi katika kukitumikia chama chao na Serikali yao na ndio maana (CCM) ikaunda Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ambao tokea kuasisiwa kwake umepata mafanikio makubwa na umekuwa muhimili muhimu wa (CCM).

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kuwa uongozi huo mpya wa (UWT) chini ya Mwenyekiti wake Gaudensia Kabaka utafanya vizuri kwa azma ya kuendeleza mafanikio katika Umoja huo na CCM kwa ujumla.

Akitoa wito kwa Umoja huo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza umoja, mapenzi na na mshikamano miongoni mwa Wanajumuiya sambama na kufanya kazi wakiwa wamoja.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa uongozi huo kuwaandaa vijana kushika nafasi za uongozi katika Umoja huo wa (UWT) hapo baadae hasa ikizingatiwa kuwa kiongozi huandaliwa hivyo ni vyema wakaandaliwa vijana watakao kitumikia chama chao cha (CCM).

Nae Mwenyekiti wa (UWT) Taifa Gaudensia Kabaka alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya (CCM) ya mwaka 2015-2020 huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kupata kura zote katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Disemba mwaka 2017.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa kupata kura zote kwa Rais Dk. Shein ambaye ni Makamo Mwenyekiti wa (CCM) Zanzibar kunatokana na kuwa (CCM) inamkubali na inazikubali kazi zake anazozifanya katika kuiongoza Zanzibar na watu wake pamoja na chama hicho.

Aidha, Mwenyekiti huyo alizipongeza juhudi za Rais Dk. Shein kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana katika kuendeleza na kuimarisha miradi ya maendeleo Unguja na Pemba sambamba na hatua alizozichukua za kuwaenzi wazee wa Zanzibar na kuwapa nafasi za uongozi akina mama katika Serikali anayoiongoza.

Pia, Mwenyekiti huyo alieleza azma, malengo pamoja na mikakati iliyowekwa katika Umoja huo katika kuhakikisha (CCM) inaendelea kushinda katika chaguzi zote ukiwemo uchaguzi ujao wa mwaka 2020 sambamba na kusisitiza mchakato wa ziara watakazozifanya Zanzibar ambazo zitaanzia kisiwani Pemba mara tu baada ya sherehe za miaka 55 za Mapinduzi mwaka huu.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Umoja wa Nchi za Falme za Kirabu (UAE) Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi Ikulu mjini Zanzibar ambapo balozi huyo ameeleza hatua zilizofikiwa na (UAE) za kuanzisha ubalozi mdogo hapa Zanzibar.

Dk. Shein kwa upande wake alipongeza hatua hizo zilizofikiwa na (UAE) za kuanzisha Ubalozi mdogo hapa Zanzibar ambazo zinatokana na mazungumzo yake aliyoyafanya kati yake na Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi na Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa (UAE), wakati wa ziara yake katika nchi za Umoja huo mapema mwaka huu.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo inaonesha wazi jinsi Umoja wa nchi hizo unavyochukua juhudi za makusudi za kuhakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo unazidi kuimarika kwa manufaa ya pande zote.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza hatua zilizofikiwa katika kuendeleza mikakati ya kukuza uchumi hapa Zanzibar na kuzipongeza nchi za Umoja huo katika hatua zake za kuiunga mkono Zanzibar ikiwemo Ras-Al-Khaimah ambayo hivi karibuni ilisaini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, kati yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Balozi Al-Marzooqi alimueleza Rais Dk. Shein hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kuanzisha Ubalozi huo mdogo hapa Zanzibar ambao alisema utazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo wenye historia.

Kiongozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Umoja wa Nchi za Falme za Kirabu (UAE) utaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo.