Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya Watu wa India Shri Ram Kovind kwa kuadhimisha miaka 74 tokea Taifa hilo kupata huru wake.Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wa Jamhuri ya India katika kusherehekea sikukuu hiyo adhimu ya uhuru wa Taifa hilo ambayo ni ya kihistoria.
Katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia Rais Ram Nath Kovind kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistori uliopo kati yake na India sambamba na kuvumbua maeneo mapya ya mashirikiano kwa maslahi ya pande zote mbili.Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo na familia yake pamoja na wananchi wote wa India afya njema na sherehe njema katika kuadhimisha siku hiyo adhimu kwa Taifa hilo na kumtakia mafanikio zaidi ya kiuchumi kwa madhumuni ya kulinufaisha Taifa hilo na wananchi wake kwa amani na utulivu mkubwa.
Jamhuri ya India inasherehekea siku ya uhuru wa Taifa hilo kila ifikapo Agosti 15 ya kila mwaka ambapo nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiengereza mnamo mwaka 1947 chini ya uongozi wa muasisi na Baba wa Taifa hilo Hayati Mahtma Gandhi.Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alimtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya Watu wa Indonesia Joko Widodo kwa kuadhimisha miaka 75 ya uhuru wa Taifa hilo.Salamu hizo za Rais Dk. Shein alizozituma kwa Rais Widodo zilieleza kuwa uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Indonesia umekuwa ukiimarika kila siku na kusisitiza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano huo kwa ajili ya kuimarisha uchumi sambamba na kupambana na changamoto zilizopo.
Bado kumekuwa na mahusiano mazuri kati ya Serikali zetu pamoja na watu wake ambao nao wamekuwa na mashirikiano na mahusiano mema kwa ajili ya kujiletea maendeleo hatua ambayo pia, imesaidia kuleta mafanikio”,alisisitiza Rais Dk. Shein.Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo sherehe njema na mafanikio katika kuadhimisha siku hii adhimu ya Uhuru wa Taifa hilo huku akimtakia afya njema, maisha marefu yeye, familia pamoja na wananchi wake sambamba na kumtakia maendeleo endelevu ya uchumi katika Taifa lake.
Jamhuri ya Indonesia inasherehekea siku ya uhuru wa Taifa hilo kila ifikapo Agosti 17 ya kila mwaka ambapo nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Uholanzi mnamo mwaka 1945 chini ya uongozi wa muasisi wake Hayati Sukarno Raden Sukami Sosrodihardjo.