Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi za Kiarabu kuwekeza Zanzibar, akibainisha kuwa Zanzibar ina mazingira bora na fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 05 Juni 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Mabalozi wa nchi za Kiarabu wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania, waliofika kwa ajili ya kumsalimia pamoja na kumpongeza kwa hatua kubwa ya maendeleo inayofikiwa na Zanzibar hivi sasa.
Rais Dkt. Mwinyi amezipongeza nchi hizo za Kiarabu kwa kuimarisha na kuendeleza uhusiano wake na Tanzania, ikiwemo Zanzibar, pamoja na misaada yao katika nyanja mbalimbali za maendeleo, ambayo ameielezea kuwa ni kichocheo muhimu cha maendeleo, ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na ushirikiano.
Aidha, amewahakikishia Mabalozi hao kuwa Zanzibar inathamini misaada inayotolewa na nchi hizo katika sekta za elimu, afya na miundombinu, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kihistoria na wa muda mrefu baina ya mataifa hayo na Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amewashauri Mabalozi hao kuzitangaza fursa zilizopo Zanzibar kwa wawekezaji na wafanyabiashara katika nchi zao ili waje kuwekeza, hususan katika sekta za utalii na uchumi wa buluu. Amesema Serikali imeandaa sera, mazingira mazuri ya uwekezaji na vivutio mbalimbali.
Rais Dkt. Mwinyi amesema sekta ya utalii, ambayo ni nguzo muhimu ya uchumi wa Zanzibar na inachangia asilimia 30 ya pato la Taifa, inaendelea kuwa na fursa za ushirikiano na uwekezaji ambazo wawekezaji kutoka mataifa ya Kiarabu wanaweza kuzitumia kwa tija na mafanikio.
Akizungumzia sekta ya uchumi wa buluu, amesema pia ni sekta muhimu yenye fursa nyingi, ikiwemo utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, utalii wa mikutano (MICE), uvuvi, utalii wa michezo, utalii wa fukwe, mazao ya baharini pamoja na fursa zilizopo katika Bandari Jumuishi ya Mangapwani.
Rais Dkt. Mwinyi amezipongeza taasisi mbalimbali kutoka nchi za Kiarabu zinazoendelea kuwekeza na kuisaidia Zanzibar katika nyanja tofauti za maendeleo, uchumi na ustawi wa jamii. Aidha, amezihakikishia taasisi hizo ushirikiano zaidi, sambamba na kuyakaribisha makampuni na wawekezaji kuwekeza Zanzibar, katika sekta za biashara na uwekezaji.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameziomba nchi hizo kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi na mkakati wake wa kuleta mageuzi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa mfumo wa kidigitali, kuwajengea uwezo watu wake kupitia mafunzo katika nyanja mbalimbali za teknolojia, pamoja na kuongeza fursa za mafunzo kwa Wazanzibari katika nchi hizo za Kiarabu.
Mabalozi waliofika Ikulu ni pamoja na:
1. Balozi wa Comoro, Mhe. Ahmada El Badaoui,
2. Balozi wa Misri, Mhe. Sharif Abdelhamid Ismail.
3. Balozi wa Saudi Arabia, Mhe. Yahya Ahmed Okesh.
4. Balozi wa Sudan, Mhe. Mohamed Abdala Abdelhameed.
5. Balozi wa Algeria, Mhe. Ghalib Zemane.
6. Balozi wa Palestine, Mhe. Salam Abuu Sharara.
7. Kaimu Balozi wa Syria, Acram Fayz Alhada.
8. Kaimu Balozi wa Yemen, Ahmad Sale Al Umar.
9. Kaimu Balozi wa Qatar, Abdulla Saeed Al Naimi.
10. Kaimu Balozi wa Somalia, Abdillatif Abdullah Hilowle.
11. Kaimu Balozi wa Libya, Ezzeddin Bahri
Akiwasilisha salamu kwa niaba ya Mabalozi hao, Balozi wa Saudi Arabia, Mhe. Yahya Ahmed Okesh, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake unaoleta maendeleo na mabadiliko makubwa katika uchumi wa Zanzibar na ustawi wa watu wake. Aidha, amesifu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ujenzi wa miundombinu, ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na bandari, pamoja na kuimarika kwa sekta ya utalii, hatua inayochochea kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaokuja Zanzibar.
