Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameupongeza Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kwa kazi nzuri na ya kujitolea waliyoifanya wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kukipatia ushindi mkubwa Chama Cha Mapinduzi.
Dkt. Mwinyi amewahakikishia vijana kuwa mambo yote aliyowaahidi wakati wa kampeni atayatekeleza kwa umakini mkubwa ili kuwawezesha vijana, huku akiutaka uongozi wa UVCCM kujipanga vema kwa ajili ya utekelezaji huo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 16 Mei 2026, alipojumuika na vijana wa CCM katika sherehe ya DKT. MWINYI UVCCM USHINDI PARTY, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Vijana wa CCM Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Aidha, ameyapongeza makundi yote ya hamasa kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uzalendo, pamoja na kukitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa ari kubwa, huku akisisitiza kuwa Chama kinajivunia kuwa na vijana walio tayari kujitolea kwa ajili ya Chama chao.
Hafla hiyo ilijumuisha dhifa ya chakula cha mchana, pamoja na burudani ya muziki wa kizazi kipya, ngoma za asili, taarabu na sanaa mbalimbali za utamaduni.
Sherehe hiyo imefanyika kufuatia ahadi aliyoitoa Makamu Mwenyekiti, Dkt. Mwinyi, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 mahsusi kwa makundi ya hamasa ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kukipatia ushindi wa kishindo Chama hicho.
