Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa usawa na kwa ufanisi. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 20 Juni 2026, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, iliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Kizimbani, Dole, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema kampeni hiyo imekuwa chachu ya kuwawezesha wananchi, hususan wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria, kupata haki bila malipo. Aidha, Serikali inalenga kuondoa vikwazo vya umbali, gharama na uelewa mdogo wa sheria kwa kufikisha huduma hadi ngazi za kata, vijiji, mitaa na shehia. Rais Dkt. Mwinyi amesema utawala bora unahitaji uwajibikaji unaosimamiwa na sheria, huku amani na utulivu wa Taifa vikitegemea haki inayotendeka, kuonekana na kupatikana kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Akizungumzia Awamu ya Kwanza ya Kampeni iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2026, amesema zaidi ya wananchi milioni nne walinufaika na huduma za msaada wa kisheria katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar. Mafanikio hayo yametokana na usimamizi madhubuti, ushirikiano na uwajibikaji wa wadau wote. Amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisera na kisheria, kuanzisha madawati ya msaada wa kisheria katika halmashauri za Tanzania Bara, pamoja na Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara ya Katiba na Sheria kinachoshughulikia malalamiko, changamoto na migogoro ya kisheria ya wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa rai kwa wizara na wadau katika mnyororo wa utoaji haki kuimarisha ushirikiano ili Awamu ya Pili iwafikie wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya pembezoni, vijana na makundi yenye mahitaji maalumu. Amesema kampeni hiyo inaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 hadi 2030, zinazoweka kipaumbele katika kujenga mfumo imara wa haki, utawala bora, amani, usalama na utulivu wa Taifa.