Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayochangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo, tarehe 18 Mei 2026, alipokutana Ikulu Zanzibar na aliyekuwa Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia Kanda ya Tanzania,Malawi,Zimbabwe na Zambia Bw. Nathan Belete, aliyefika kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi pamoja na kumtambulisha Mkurugenzi Mpya, Bw. Firas Raad.

Amesema ushirikiano kati ya Zanzibar na Benki ya Dunia umeleta mafanikio makubwa katika sekta za elimu, afya, miundombinu na maendeleo ya rasilimali watu, huku akiomba Benki hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya afya, nishati na miundombinu ya barabara kupitia mradi wa BIG-Z.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameshauri Benki ya Dunia kufungua ofisi Zanzibar ili kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Kwa upande wake, Bw. Nathan Belete ameihakikishia Zanzibar kuendelea kwa ushirikiano mzuri wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.