Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras) kutumia elimu, maarifa na ubunifu wao kutatua changamoto za jamii, kuboresha maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo endelevu.
Akizungumza akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 63 ya IIT Madras, yaliyofanyika leo, tarehe 17 Julai 2026, jijini Chennai, India, Rais Dkt. Mwinyi amesema elimu ni msingi wa kujenga taifa, kuimarisha jamii na kuandaa kizazi chenye maarifa, ujasiri na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya.
Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwekeza katika elimu ya juu, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nguzo muhimu za utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa na Ajenda ya Uchumi wa Buluu.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Kampasi ya IIT Madras Zanzibar imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kielimu kati ya Tanzania na India, huku ikitoa fursa kwa vijana wa Afrika kupata elimu ya kiwango cha kimataifa na kuimarisha utafiti, ubunifu na ujasiriamali.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameshiriki kuwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu ya juu, akiwemo wa shahada ya kwanza na shahada ya uzamivu (PhD). Aidha, alikabidhiwa Tuzo Maalum kutoka IIT Madras kwa kutambua mchango wake katika kuanzishwa na kuendelezwa kwa Kampasi ya IIT Madras Zanzibar.
Mahafali hayo pia yaliambatana na uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kampasi mpya ya kudumu ya IIT Madras Zanzibar, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi nafasi ya Zanzibar kama kitovu cha elimu, utafiti na teknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa, Mkurugenzi wa IIT Madras, Profesa V. Kamakoti, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Kapufi Mbega, Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey, pamoja na Viongozi mbalimbali, Wahadhiri, Wazazi na Familia za Wahitimu.
.jpeg)