Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar itaendelea kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na Ireland, hususan katika sekta za uwekezaji, biashara, uchumi wa buluu, utalii na ustawi wa jamii.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 30 Aprili 2026, alipokutana na Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Balozi Nicola Brennan, Ikulu Zanzibar, ambapo pia ameishukuru Ireland kwa mchango wake katika sekta za afya, elimu na sheria.

Aidha, amewakaribisha wawekezaji kutoka Ireland kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta mbalimbali za maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuhifadhi Mji Mkongwe kama urithi wa kihistoria na kivutio cha utalii.

Kwa upande wake, Balozi Brennan amepongeza maendeleo ya Zanzibar na kuahidi kuendeleza ushirikiano pamoja na kuongeza fursa za mafunzo, hususan katika sekta ya sheria.