Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa wananchi wa Tanzania kuufanya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria kuwa mwaka wa maridhiano, upendo na ustahamilivu. Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo, tarehe 15 Juni 2026, katika Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria, yaliyofanyika katika Msikiti wa Jamiu Zinjibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amewahimiza wananchi, kuheshimiana na kulinda maadili, kusaidiana, pamoja na tunu ya amani, ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa na kuwataka wananchi kujiepusha na mambo yote yanayoweza kuwagawa. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuhimiza umoja wa kitaifa, kuimarisha maadili, kukuza amani na kujenga jamii yenye ustawi.

Ameeleza kuwa Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na taasisi za dini katika kuhimiza mambo mema na maadili, ambayo ndiyo msingi wa mustakabali bora wa jamii. Rais Dkt. Mwinyi amesema jamii haiwezi kuwa na maendeleo bila maridhiano, na haiwezi kuwa na maridhiano bila ustahamilivu.

Amepongeza kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema, “Hijra ni Chimbuko la Maridhiano katika Jamii.”
Amewanasihi waumini wa Dini ya Kiislamu kutokata tamaa wanapokabiliwa na changamoto, bali kuwa na subira, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kufuata maadili mema ili kufanikiwa duniani na Akhera.

Alhaj Dkt. Mwinyi amempongeza Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, Baraza la Maulamaa na viongozi wote wa dini nchini kwa mchango wao katika kudumisha amani, umoja na ustawi wa jamii.

Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, kwa kushirikiana na Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho hayo. Pia, amewashukuru viongozi wa Dini ya Kiislamu kutoka nchi za Afrika Mashariki walioshiriki na kutoa mada muhimu katika maadhimisho hayo.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza tarehe 17 Juni 2026 kuwa siku ya mapumziko kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria.