Mke wa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti na Msarifu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha ustawi wa jamii, kuwawezesha vijana na wanawake, pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Juni 2026, wakati alipofanya mazungumzo na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Jane Ittogi Shanmugaratnam, aliyetembelea ofisi za Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation zilizopo Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza mipango yake kwa mafanikio kutokana na kuungwa mkono na jamii inazozihudumia, wadau pamoja na washirika wake, ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa ushirikiano kati ya taasisi hiyo na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya kuwawezesha wasichana, vijana na wanawake, kuimarisha afya ya akili, kukuza usawa wa kijinsia na kuongeza fursa za ajira.

Mama Mariam Mwinyi amemshukuru Mke wa Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Jane Ittogi Shanmugaratnam, kwa kutembelea taasisi hiyo na kupata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kwa lengo la kuwasaidia na kuwawezesha wananchi wa Zanzibar.

Naye Mke wa Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Jane Ittogi Shanmugaratnam, ameipongeza Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii kupitia programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wasichana, vijana na wanawake, pamoja na kukuza fursa za maendeleo.

Halikadhalika, Mhe. Jane Ittogi Shanmugaratnam amesifu mapokezi mazuri yaliyoandaliwa na taasisi hiyo, pamoja na fursa ya kutembelea na kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Zanzibar Maisha Bora Foundation.

Wakati huo huo, Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi, amemtunukia zawadi ya heshima Mke wa Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Jane Ittogi Shanmugaratnam, na kumhakikishia kuendelezwa kwa ushirikiano baina yao.