Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inakusudia kufungua ukurasa mpya wa uhusiano na ushirikiano na Jamhuri ya Singapore, hususan katika diplomasia ya uchumi, biashara na uwekezaji. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Juni 2026, alipozungumza na Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Tharman Shanmugaratnam, ambaye yupo Tanzania kwa ziara ya siku tatu. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amesema uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo rafiki sasa unapaswa kuelekezwa katika kuibua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi yatakayoleta manufaa zaidi kwa pande zote mbili. Amesema Zanzibar inatarajia kuimarisha ushirikiano huo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kubadilishana uzoefu, ujuzi, elimu, teknolojia, maarifa mapya, kujenga uwezo wa nguvu kazi na kufanya kazi kwa pamoja katika sekta za kimkakati za biashara na uwekezaji.

Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Singapore kuwa Zanzibar itaendelea kudumisha uhusiano wa kidugu uliopo baina ya pande hizo mbili, aliouelezea kuwa ni nyenzo muhimu ya kuwaleta pamoja wananchi wa Zanzibar na Singapore. Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameyakaribisha makampuni, wawekezaji na wafanyabiashara wa Singapore kuwekeza Zanzibar katika sekta kuu za uchumi wa buluu na utalii.

Akizungumzia sekta ya uchumi wa buluu, Rais Dkt. Mwinyi amesema sekta hiyo ina fursa nyingi za uwekezaji, ambapo Zanzibar inahitaji wawekezaji makini katika maeneo ya mafuta na gesi asilia, uvuvi wa bahari kuu, pamoja na usindikaji wa mazao ya baharini. Ameeleza kuwa tafiti za awali zimeonesha kuwepo kwa viashiria vya nishati katika baadhi ya maeneo ya Zanzibar, hali inayofungua fursa mpya za uwekezaji katika eneo hilo muhimu la kimkakati.

Kuhusu kilimo cha mwani, Rais Dkt. Mwinyi amesema zao hilo limebeba wananchi wengi wanaojishughulisha na kilimo hicho, hivyo Zanzibar inahitaji uwekezaji wa viwanda vya kuliongezea thamani ili kuondokana na utaratibu wa kusafirisha mwani kama malighafi. Akizungumzia sekta ya nishati, Rais Dkt. Mwinyi amesema nishati ya umeme ni eneo jengine muhimu ambalo Zanzibar inahitaji wawekezaji, kutokana na ukuaji wa sekta ya utalii, ongezeko la hoteli na miradi mikubwa ya uwekezaji.

Rais Dkt. Mwinyi pia ameishawishi Singapore kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za mageuzi ya teknolojia na mifumo ya kidigitali, ikiwemo utoaji wa huduma za kidigitali katika taasisi za umma, kuwajengea uwezo watendaji na kuendeleza fursa za mafunzo kwa Wazanzibari nchini Singapore. Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameielezea ziara ya Rais Tharman Shanmugaratnam hapa Zanzibar kuwa ni kielelezo cha kuanza kwa awamu mpya ya uhusiano na ushirikiano, pamoja na kuibua fursa mpya za maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Naye Rais wa Singapore, Mhe. Tharman Shanmugaratnam, amesema nchi yake inakusudia kuimarisha zaidi ushirikiano na Zanzibar na kuunga mkono juhudi zake za kujiletea maendeleo. Rais Tharman ameisifu Zanzibar kwa mageuzi makubwa ya kimaendeleo yanayoonekana hivi sasa, na kuahidi kuhamasisha wawekezaji wa Singapore kuja kuwekeza Zanzibar.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi, alimwandalia mgeni wake, Rais Tharman dhifa ya chakula cha mchana iliyofanyika Ikulu Zanzibar.