RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa Serikali anayoiongoza imekuwa ikitekeleza ahadi inazoziahidi, hivyo ujenzi wa barabara ya Magogoni kwa Mabata hadi Kinuni ni ahadi ambayo hivi sasa inatekelezwa kwa vitendo.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa ,kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara
Maalum za SMZ ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 3.62.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa barabara hiyo imejengwa katika kipindi hichi kutokana na ahadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo iliahidi
kujenga barabara hiyo katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020.

Alieleza kuwa wapo waliozania ni utani, wapo waliofanya kejeli na kila mmoja alisema lake lakini wapo waliotambua kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaijenga barabara hiyo tena kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidi.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoka pongezi kwa Kampuni ya MECO inayojenga barabara hiyo ambayo imepewa miezi sita kuijenga lakini badala yake imeahidi itaijenga ndani ya miezi miwili.

Aidha, Dk. Shein alikubali ombi la wananchi katika maeneo hayo walilomuomba katika hafla hiyo kuwa barabara yao hiyo ijengwe hadi Kijitoupele ili izidi kuwasaidia.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Radhia Rashid Haroub alieleza kuwa barabara hiyo ni moja wapo ya barabara za ndani ambazo zimetengewa TZS bilioni 1.53 na kueleza kuwa bilioni 1.2 zmetengwa kwa ajili ya barabar hiyo.


Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umezingatia vigezo na ubora wa kutosha ikiwemo vituo vya kupandia na kushushia abiria, misingi ya maji mifupi na mirefu, alama za barabara pamoja na matuta kwa ajili ya kuepusha ajali.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza na kutoa wito kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo kufuata sheria na taratibu za barabara kwani itatumiwa na watu mbalimbali
wakiwemo wazee, watoto, wagonjwa pamoja na watu wenye ulemavu.

Wakati huo huo, Dk.Shein aliweka jiwe la msingi katika Skuli ya Msingi ya Kijitoupele na kutoa pongezi kwa Mkoa wa Mjini Magharibi chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wake Ayoub Mohammed kwa kuanzisha kampeni ya ‘Mimi na Wewe’, Kampeni ambayo imesaidia kupatikana kwa TZS milioni 70.6 zilizojenga madarasa hayo matatu pamoja na Maktaba kwa muda wa siku 11.

Dk. Shein alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Mikoa mingine kuiga Kampeni hiyo ya Mimi na Wewe ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha miradi ya
maendeleo.

Rais Dk. Shein alieleza juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Srerikali anayoiongoza katika kuimarsha sekta ya elimu kwa kushirikiana na Washirika
wa Maendeleo wakiwemo nchi za Jamhuri ya Watu wa China na Korea Kusini ambazo zinampango wa kujenga skuli za ghorofa huko Kwarara na Fuoni Mambo sasa.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja kwa viongozi katika kuwatumikia wananchi kwani kiongozi huchaguliwa na wananchi hivyo ni vyema akawatumikia wananchi na sio kuwatilia mbwembwe.

Dk. Shein alielendelea na ziara yake katika Mkoa huo wa Mjini kwa kukagua maendeleo ya mradi wa nyumba huko Nyamanzi ambapo alipongeza hatua za mradi huo ambao utakapokamilika utaongeza haiba ya mji wa Zanzbar.

Akiwa katika eneo hilo linalojengwa nyumba zikiwemo zile za teknolojia ya mbao ambazo hazitumii mchanga mwingi wala kokoto, ambapo malighafi hizo hutumika kwa kujengee msingi tu pamoja na nyumba za ghorofa ambapo tayari miongoni mwao zimeshanunuliwa kwa mujibu wa maelezo ya Meneja Mkuu wa Mradi huo Sebastian Dietzolt.

Muhandisi wa Mradi huo Akif Ali Khamis alimueleza Dk. Shein juu ya umadhubuti wa nyumba hizo ambazo huchukua muda wa siku saba kutengenezwa na hutumia siku moja kwa ajili ya kuwekwa eneo husika ambapo haziathiriki na maji wala moto.

Pia, Dk. Shein aliweka jiwe la Msingi, Maskani ya Tuko Imara iliyopo Bweleo na kueleza haja kwa viongozi pamoja na wanaCCM katika kutekeleza Ilani ya chama hicho ili kizidi kuimarika.

Akimaliza ziara yake, Dk. Shein alipata nafasi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba huko Fumba na kupata fursa ya kukagua eneo lililojengwa kwa ajili ya mapumziko ambalo lina sqm 50,000 ambapo tayari kumeshawekwa taa, kumepandwa miti pamoja na huduma nyengine muhimu.

Mwakilishi wa Kampuni ya Bakhressa Group of Companies, Salim Aziz alimueleza Dk. Shein kuwa mradi huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara yenye kilomita 25 ambapo tayari kilomita 18 ziko tayari  na kilomita 10.2 zimeshawekwa lami na zina huduma zote za kupitisha umeme na maji.

Alieleza kuwa eneo hilo lina nyumba 70 ambapo miongoni mwa hizo 8 ziko tayari na wageni wanakwenda na kuonesha hamu kubwa ya kuzinunua na kwa mashirikiano na Mamlaka ya Uwekezaji wa Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Dk. Shein alipata fursa ya kujibu masuali ya waandishi waliokuwemo katika ziara hiyo na kuwaeleza kuwa kumekuwepo mashirikiano makubwa kati ya sekta
binafsi na serikali kwani sekta binafsi ni nguzo katika maendeleo.