Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Msarifu wa Benjamin William Mkapa Foundation (BMF), Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameongoza Harambee ya Mfuko wa Wakfu wa BMF iliyokusanya ahadi za michango yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.65, kuvuka lengo la awali la Shilingi bilioni moja.
Harambee hiyo imefanyika leo, Novemba 12, 2026, katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kujenga mtaji wa kudumu utakaowezesha BMF kuendeleza programu za afya, ikiwemo mafunzo ya madaktari na wauguzi pamoja na kuimarisha huduma za afya nchini.
Katika harambee hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuchangia Shilingi milioni 123, huku Gazeti la Mwananchi na Malkia Choice zikiahidi kutoa huduma za matangazo zenye thamani ya Shilingi milioni 50, na Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) likiahidi kutoa tiketi 50 kusaidia shughuli za BMF.
Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza wadau wote waliojitokeza kuunga mkono Mfuko huo wenye lengo la muda mrefu la kufikia Shilingi bilioni 33.7, katika kuendeleza maono na urithi wa Hayati Rais Benjamin William Mkapa.
