Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ziara ya Waziri wa Mambo ya Kale na Utalii wa Oman, Mhe. Sayyid Ibrahim bin Said Al Busaidi, inaonesha dhamira ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria na ushirikiano baina ya Zanzibar na Oman.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 13 Novemba 2026, alipokutana na Waziri huyo Ikulu Zanzibar, akisisitiza umuhimu wa kutekeleza Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa baina ya nchi hizo katika kuendeleza utalii, kuhifadhi urithi wa kihistoria, kuvutia uwekezaji na kubadilishana utaalamu.

Amesema ushirikiano huo utafungua fursa mpya katika utangazaji na masoko ya utalii, ukarabati wa maeneo ya kihistoria, makumbusho, tafiti na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Kwa upande wake, Waziri Al Busaidi ameeleza utayari wa Oman kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza sekta za utalii na urithi wa kihistoria, kwa kuzingatia historia na uhusiano wa muda mrefu unaounganisha pande hizo mbili.