RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,  ameeleza kuwa ujenzi wa majengo bora ya Serikali ni azma iliyoanza mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 1964.

Akinukuu maelezo ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Rais Dk. Shein alisema kuwa nchi inaendelea kwa kujengwa majengo na ndio maana Awamu ya Saba nayo inatekeleza hatua hiyo.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya ufunguzi wa jengo la Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati pamoja na Taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA), huko Maisara, Jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa Awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilifuata mkondo huo ambapo kila Awamu ilijenga majengo bora na ya kisasa mjini na vijijini.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina historia kubwa katika ujenzi wa majengo yakiwemo yale iliyoyajenga wenyewe kwa kupitia wataalamu na wajenzi wazalendo yakiwemo majumba ya Michenzani, Kilimani, Mpapa, Kikwajuni, Mkoani, Wete na Chake Chake kwa kupitia Idara maalum ya ujenzi iliyokuwa chini ya SMZ.

Alisema kuwa ujenzi wa kutegemea wataalamu wa nje unaviza elimu na utaalamu wa wajenzi wazalendo na kueleza nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Kampuni ya Ujenzi yake wenyewe ambayo tayari imeshaanza kazi.

Aliongeza kuwa Kampuni hiyo ishaundwa kwa lengo la kujenga majengo bora na ya kisasa ambayo itawashirikisha wataalamu na mafundi kutoka Idara za Vikosi vya SMZ na pale itakapoonekana haja ya kukaribishwa Kampuni za nje zitakaribishwa.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Kampuni hiyo itajengewa uwezo na kwa kuanzia itaanza kujenga majengo ya hospitali ya Binguni, iliyopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakwenda na wakati licha ya kuwepo watu ambao hawapendi pale inapofanya mambo mazuri huku akirejea kauli yake ya kukemea vikali wale walioharibu miundomnibu ya taa za barabarani kwa kuzivunja kwa makusudi huko kisiwani Pemba.

Alisisitiza kuwa waliofanya hivyo wana matatizo ya akili kwani si rahisi kwa mtu mwenye akili zake timamu akaharibu kwa makusudi taa za barabarani ambazo zinawasaidia wananchi wote.

Sambamba na hayo Rais Dk. Shein alisema kuwa mwelekeo wa matokeo ya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia unakwenda vizuri na taarifa maalum itatolewa baada ya Kampuni ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) na RAK Gas ya Ras Al Khaimah kumaliza kazi waliyopewa.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina uwezo mkubwa na ikiamua kufanya mambo yake wenyewe inafanya tena bila ya kuwezeshwa kama ilivyofanya kwa ujenzi wa jengo hilo ambapo fedha zote ni za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya kazi kwa pamoja na hatimae kupata mafanikio hayo huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Wizara hiyo pamoja na uongozi wote wa Wizara.

Pia, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) na kueleza jinsi inavyofanya kazi vizuri ikiwa ni pamoja na kuonesha matokeo ya Mamlaka hiyo katika ujenzi wa bandari ya Mangapwani pamoja na nyumba 31 kwa ajili ya wananchi waliopisha ujenzi huo ambao watapewa bure.

Rais Dk. Shein pia, aliipongeza Kampuni ya ujenzi ya Hainan Internationa Limited.

Nae Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib alimshukuru na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa niaba ya wafanyakazi na uongozi wa Wizara hiyo kwa kujenga jengo hilo sambamba na miongozo aliyokuwa akiitoa.

Alieleza kuwa licha ya baadhi ya changamoto zilizotokea lakini mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kumaliza ujenzi wa jengo hilo kwa wakati huku akieleza sehemu za jengo hilo ukiwemo ukumbi mkubwa na wa kisasa walioupa jina la “Dk. Shein Conference Hall”.
Mapema,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Ali Khalil Mirza alisema kuwa gharama zote za ujenzi wa jengo hilo zimetolewa na SMZ ambazo ni Tsh. Bilioni 19.9.

Aliongeza kuwa ghorofa 7 za juu ya ardhi za jengo hilo zitatumika kwa shughuli za kiofisi kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati pamoja na Taasisi zake zikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA), Mamlaka ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA), Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) na Idara ya Nishati na Madini.

Alieleza kuwa ghorofa iliyoko kwenye usawa wa ardhi imepangwa kutumika kwa shughuli za kibenki na tayari uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) inakamilisha taratibu za kuweza kuanza kutoa huduma.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa ghorofa iliyopo chini ya ardhi ni kwa ajili ya kuegesha vyombo vya usafiri vya wafanyakazi watakao tumia jengo hilo ambapo zinakadiriwa kuwa maegesho 40.

Katibu Mkuu huyo alitoa pongezi na shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi zake alizozichukua za kuhakikisha kuwa kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi Wizara hiyo inahamia katika jengo lake jipya kama ilivyo kwa Wizara nyengine za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

  • Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein  akizungumza na Viongozi mbali mbali Wananchi na wafanyakazi wa  Wizara ya Ardhi,Nyumba,Maji na Nishati katika hafla ufunguzi wa jengo jipya la Wizara hiyo leo Maisara Mjini ZanzibRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Viongozi mbali mbali Wananchi na wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi,Nyumba,Maji na Nishati katika hafla ufunguzi wa jengo jipya la Wizara hiyo leo Maisara Mjini Zanzib