RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezitaka taasisi za ZAWA, ZECO na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kufanyakazi kwa karibu na wakandarasi wanaojenga barabara ili kukabiliana na tatizo la uharibifu wa miundombinu ya maji, umeme na huduma nyengine kwa wananchi.Alhajj Dk. Mwinyi, ametoa kauli hiyo alipohutubia kwenye Baraza la Eid huko ukumbi wa Chuo cha Polisi – Ziwani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema, wakati wa zoezi la ujenzi wa barabara hizo likiendelea, kumeibuka changamoto nyingi, hivyo alizitaka taasisi hizo kushirikiana kudhibiti uharibifu huo.Akiuzungumzia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa waumini wa dini ya kiislam, Alhajj Dk. Mwinyi alisema waumini hao wana kila sababu ya kujifunza uchamungu na maisha ambayo Mwenyezi Mungu (S.W) anawataka waishi hapa duniani.

“Tulitekeleza vyema ibada ya saumu kwa ikhlas tukitaraji malipo mema kama alivyotuahidi Mwenyezi Mungu, tulijitajidi kusali sala za fardhi kwa wakati na sala za sunna kwa wingi, kusoma sana Quran ambapo tulishuhudia darsa nyingi zikiendeshwa misikitini pamoja na kuwepo kwa mashindano kadhaa ya kuhifadhi Quran katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.” Alieleza Allhajj Dk. Mwinyi.

Aidha, Alhajj Dk. Mwinyi alisifu jitihada za waislamu pamoja na taasisi mbali mbali kwa kutoa sadaka kwa makundi tofauti yenye uhitaji wakiwemo yatima, wajane, wazee na masikini suala aliloeleza kwamba liliongeza mapenzi, kuhurumiana, umoja, mshikamano, amani na mashikamano nchini.Alisema, darasa mbalimbali zilitoa mafundisho ya kubadili mienendo ya watu kwenye maisha yao ya kila siku.

Akizungumzia suala la amani na utulivu uliopo nchini, Alhajj Dk. Mwinyi alieleza imesaidia watu kutekeleza ibada zao kwa uhuru, usalama, pamoja na kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo.Akizungumzia sikukuu ya Eid el Fitri pamoja na harakati za viwanja vya sikukuu hasa kwa matumizi ya usafiri wa barabara, Alhajj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuliagiza Jeshi la Polisi nchini, kushirikiana na Ofisi za Mikoa na Wilaya pamoja na vyombo vyote vya usalama kuimarisha ulinzi na usalama kwa maeneo yote ya sikukuu pamoja na kuwataka wananchi kusherehekea sikukuu kwa amani na utulivu.

Pia, Alhajj Dk. Mwinyi aliendelea kulihimiza taifa kudumisha amani kwa kila hali ili nchi izidi kupiga hatua za maendeleo sambamba na kuwaomba Viongozi wa dini, Masheikh na walimu kuendelea kuiombea dua nchi na viongozi wazidi kuwa na amani, washirikiane kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za maendeleo zinazoikabili nchi na watu wake.