Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa kujenga skuli za kisasa zenye hadhi, viwango na ubora unaokidhi mahitaji ya elimu ya karne ya sasa. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 10 Januari 2026 alipofungua Skuli mbili za Ghorofa za Ramadhan Haji Faki iliyopo Gamba, Mkoa wa Kaskazini Unguja, pamoja na Skuli ya Kifundi ya kwa niaba iliyopo Pemba.
Amesema ujenzi wa skuli hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuondokana na skuli za mabanda na badala yake kuwa na majengo ya kudumu yanayokidhi viwango vya kisasa vya elimu, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi wa ufundishaji na mafunzo. Aidha, amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kutumia kikamilifu fursa ya miundombinu bora iliyowekezwa na Serikali.
Akizungumzia ujenzi wa dakhalia, Rais amesema utasaidia kumaliza changamoto ya wanafunzi kukaa nje ya mazingira ya skuli, hali ambayo imekuwa ikichangia kushusha uwezo wao wa kitaaluma, na kuwasisitiza wanafunzi kutumia fursa hiyo kufanya vizuri katika masomo yao.
Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa Skuli ya Gamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ndg. Khamis Abdalla Said, amesema skuli hiyo imegharimu Shilingi Bilioni 11.2 na imejengwa na Kampuni ya ZECON, ikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 800 kwa wakati mmoja. Ameongeza kuwa Skuli ya Kifundi ya Pemba imegharimu Shilingi Bilioni 9.4 na imejengwa na Kampuni ya SALEM Construction.
Skuli hizo zimejengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA), kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha sekta ya elimu na kukuza rasilimali watu Zanzibar.
