Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameyakaribisha makampuni na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Ufaransa kuja kuwekeza Zanzibar, hususan katika sekta kuu za uchumi zikiwemo Utalii na Uchumi wa Buluu.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema leo, tarehe 27 Februari 2026, alipokutana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Anne-Sophie, aliyefika Ikulu, Zanzibar kwa mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Ufaransa.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji wawekezaji makini na wenye mitaji mikubwa watakaowekeza katika sekta hizo muhimu ili kuimarisha nguvu kazi, kuongeza utaalamu pamoja na kuboresha utoaji wa huduma, hasa katika sekta ya utalii na maendeleo ya uchumi wa buluu.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Ufaransa kuwa Zanzibar iko tayari kuendeleza na kupanua zaidi fursa za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya kidiplomasia na kiuchumi.Amewasisitiza wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kubaini na kutumia fursa nyingi za uwekezaji zilizopo.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha sera bora za uwekezaji pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kisasa ikiwemo barabara na bandari. Ameitaja Bandari Jumuishi ya Mangapwani kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo itakapokamilika itatoa fursa nyingi za uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi. Pia amesisitiza azma ya Serikali ya kukiendeleza Kisiwa cha Pemba kuwa kituo cha uwekezaji na utalii endelevu.

Kwa upande wake, Balozi Anne-Sophie ameihakikishia Zanzibar kuwa Ufaransa itaendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta muhimu za kiuchumi.

Ameeleza kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana katika miradi ya sekta ya utalii, afya, elimu, utamaduni, maendeleo ya Mji Mkongwe, mazingira pamoja na uchumi wa buluu