Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameendelea kuwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu wenye uwezo kuwasaidia watu wasio na uwezo, hususan katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili nao waweze kutimiza ibada ya funga ipasavyo.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Februari 2026, alipoungana na waumini katika Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Fatma Bint Mirdas uliopo Kilimani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza kuwa ndani ya jamii kuna makundi ya watu masikini, mafakiri, watu wenye ulemavu, wajane na mayatima wanaohitaji kuhurumiwa na kusaidiwa zaidi katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani, na kuisisitiza jamii kutimiza wajibu huo kwa moyo wa huruma na mshikamano.
Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amewataka wafanyabiashara kuepuka kupandisha bei za bidhaa za vyakula, akibainisha kuwa Mwezi wa Ramadhani si kipindi cha kutafuta faida kubwa bali ni wakati wa kuhurumiana, kusaidiana na kuonesha utu.
Ameongeza kuwa ni busara kwa wafanyabiashara kushusha bei au kuziendeleza kwa kiwango cha kawaida, badala ya kupandisha bei na kuwafanya baadhi ya wananchi kushindwa kumudu kununua mahitaji ya futari.
