Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi alipozindua Duru ya kwanza ya utoaji wa vitalu kwa kampuni kwenye maeneo ya bahari kwa Zanzibar.Alisema, katika utekelezaji wa dhana ya Uchumi wa Buluu, Serikali inatoa fursa kubwa kwa wawekezaji wa sekta ya Mafuta na Gesi Asilia na kuwahakikishia mazingira rafiki ya utekelezaji wa shughuli hizo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa eneo la Zanzibar limepata sifa ya kutambulika kuwa ni mahali pazuri kwa makampuni kuwekeza kwani ni maeneo salama.Pia, alisema Serikali inaamini fursa zinazotokana na Uchumi wa Buluu zitakuza mipango ya maendeleo ya uchumi yenye lengo la kupunguza umaskini na kutengeneza ajira nyingi nchini.

Vile vile Rais Dk. Mwinyi alieleza dhamira ya Serikali kuzindua duru ya kwanza ya utoaji wa Vitalu, awali ilifanya mapitio ya mifumo ya sheria na mikataba ya Mafuta na Gesi Asilia ili kuvutia uwekezaji, iliolenga kuimarisha masharti ya fedha sambamba na kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya mafuta na gesi Asilia Zanzibar.

Dk. Mwinyi pia alieleza matarajio yake mara baada ya uzinduzi huo, kwamba utasaidia kufungua na kuharakisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwenye vitalu hivyo vipya vya baharini na hatimae kuitangaza Zanzibar kuwa sehemu ya uwekezaji wa mafuta na gesi asilia.Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wawekezaji wote wa sekta ya mafuta na gesi pamoja na sekta nyengine za uchumi kwamba, Serikali iko tayari kuwawekea mazingira mazuri ya uwekezaji kwa taifa kwa ujumla.

Naye, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman alisema Sekta ya Uchumi wa Buluu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni miongoni mwa maeneo makuu ya vipaumbele vyake. Shughuli za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar, zilianza tangu miaka ya 1950 kwa kampuni ya mafuta ya British Petroleum (BP) kushirikiana na Kampuni ya Shell zilipofanya uchunguzi wa kina na kuchimba visima viwili kwa visiwa vya Zanzibar vilivyokamilika baadae mwaka 1963 na kutoa msingi mzuri wa kuendeleza shughuli za Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar.

Mwaka 1964, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zilikua chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) na kufanikiwa kufanya tafiti mbalimbali.Aidha, hatua mpya ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi Zanzibar ilianzishwa mwaka 2015 kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Petroli Na 21 ya mwaka 2015 ya Tanzania iliyoiruhusu kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia shughuli za Mafuta na Gesi Asilia wenyewe.