RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiomba Serikali ya Marekani kusaidia juhudi za Serikali katika uzalishaji na kuliongezea thamani zao la Mwani.Dk. Mwinyi ametoa rai hiyo Ikulu Zanzibar alipozungumza na Naibu Waziri wa Wizara ya kilimo ya Marekani Dr. Jewel Bronaugh aliefika Ikulu na ujumbe wake kwa mazungumzo.

Amesema kupitia Sera ya Uchumi wa Buluu, Serikali inalenga kuimarisha kitaalamu uzalishaji wa zao la mwani ili kuliongezea thamani na kuwaletea tija wakulima, akibainisha akinamama ndio wakulima wakubwa wa kilimo hicho.Alisema Zanzibar ni nchi yenye ardhi ndogo ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikizalishaji zao la karafuu.Dk. Mwinyi alisema Serikali inakusudia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa ajira kwa vijana kupitia sekta ya uvuvi akibainisha sekta hiyo ina mchango mkubwa wa kufanikisha hilo pale itakapokuwa na mfumo bora wa uvuvi na uchakataji.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele katika uimarishaji wa miundo mbinu ya kiuchumi kwa kuviimarisha Viwanja vya Ndege vya Unguja na Pemba pamoja na Bandari.Aidha, alimueleza Naibu Waziri huyo kuwa kuwepo muundo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa hapa nchini kumefungua milango ya Uwekezaji kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo ya Utalii, hivyo akatumia fursa hiyo kutoa wito kwa watalii wa Marekani kuja nchini, huku akisifia juhudi za serikali katika uimarishaji wa miundombinu pamoja kuwepo kwa vivutio vingi vya utalii. 

Aliishukuru Serikali ya Marekani kwa mashirikiano yake ya muda mrefu na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na misaada mbali mbali ambapo nchi hiyo imekuwa ikiisaidia Zanzibar, ikiwemo ile inayopitia Shirika la misaada la   ‘USAID’.

Nae, Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo ya Marekani Dr. Jewel Bronaugh aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano yake na Marekani na kuahidi kuendeleeza ushiirikiano huo kwa faida ya nchi mbili hizo.Alisema lengo la ziara yake hapa nchini ni kukuza ushirkiano wa kibiashara kati ya Zanzibar na Marekani, ambapo wafanyabiashara wa nchi hiyo watapata nafasi ya kuangalia fursa kupitia sekta za kilimo na utalii.

Aidha, alisema Serikali ya Marekani ipo tayari kusaidia juhudi za Serikali katika uimarishaji wa maeneo mbali mbali ya kiuchumi.