Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameondoka nchini leo kuelekea Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E) kwa ziara ya siku tatu.Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi aliagwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, vyama vya siasa, dini pamoja na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla.

Ziara hiyo ya Rais Dk. Mwinyi ni kufuatia mwaliko maalumu wa Kiserikali aliopewa na Mrithi wa Mtawala wa Abudhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan.

Rais Dk. Mwinyi anatarajia kuanzia ziara yake hiyo nchini Abudhabi ambako atahudhuria Maadhimisho ya wiki Maalum ya Kushajihisha Maendeleo endelevu inayoadhimishwa kila mwaka nchini humo iliyoazia tangu mwaka 2008 pamoja na kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Nchi na Serikali mbali mbali duniani utakaofanyika huko nchini Dubai.

Katika ziara hiyo, Rais Dk. Mwinyi amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Husein Ali Mwinyi anatarajiwa kurejea nchini Jumatano, tarehe 19 Januari 2022.