Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amelishukuru Shirika la Viwango Duniani kwa kuendelea kulijengea uwezo Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS), hatua inayolisaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na ujumbe wa Shirika hilo, ukiongozwa na Rais wake Dkt. Sung Hwan Cho, uliofika Ikulu kwa mazungumzo leo tarehe 24 Juni 2025.

Aidha Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa Shirika hilo kufanya kazi kwa ukaribu na ZBS pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kuhakikisha taasisi hizo zinatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa katika kusimamia ubora wa viwango.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amelishauri Shirika hilo kuendeleza misaada ya kitaalamu kwa taasisi hizo pamoja na kuwajengea uwezo watendaji wao, ili kuwaongezea taaluma na ujuzi unaohitajika katika sekta ya viwango.Rais Dkt. Mwinyi amelipongeza Shirika la Viwango Duniani kwa uamuzi wake wa kushiriki kikamilifu katika Mkutano Mkuu wa Viwango Afrika, unaotarajiwa kufanyika Zanzibar kesho tarehe 25 Juni 2025.

Naye Rais wa Shirika la Viwango Duniani (ISO), Dkt. Sung Hwan Cho, amesifu ushirikiano uliopo baina ya Shirika hilo na ZBS na kuahidi kuendeleza uhusiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.Kwa upande wake, Rais wa Shirika la Viwango Afrika (ASO) ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Viwango la Ghana, Profesa Alex Doddoo, amesema umefika wakati kwa Afrika kuwa na viwango vyake vyenyewe ili kukabiliana na vikwazo vya kibiashara duniani.