Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza hatua na mwendelezo wa ujenzi wa viwanja vya michezo, Amani.Dk. Mwinyi, alitoa pongezi hizo alipofanya ziara za kukagua viwanja hivyo kuangalia hatua za ujenzi unavyoendelea.

Amesema, lengo la ziara yake viwanjani hapo ni kukagua maendeleo ya ujenzi wa viwanja hivyo, kwani kuna matarajio makubwa ya kufanyika kwa sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar mwezi Januari mwakani mara baada ya mkandarasi (Kampuni ya Orkun) kutoka Uturuki kuvikabidhi viwanja hivyo kwa Serikali mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu.

“Kama mnavyotambua lengo letu ni sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar mapema mwakani Januari 12, zifanyike uwanjani hapa na kwa sababu muda uliobakia ni mchache, nimeona bora nije mwenyewe nione wapi tumefikia na kama adhma yetu hiyo itafikiwa” alieleza Rais Dk. Mwinyi.Aidha, alisifu mwendelezo wa ujenzi wa uwanja huo unavyoendelea na kueleza, uwanja una kiwango kilichokubalika na Serikali na kwamba sehemu ndogo iliyosalia hadi kukamilika kwake.

Pia Rais Dk. Mwinyi alieleza,  ni jambo la faraja kwa Serikali endapo uwanja huo utakamilika kwa wakati, sababu ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliobaki kuna changamoto kadhaa ikiwemo mvua zinazoendelea kunyesha na changamoto za bandarini wakati wa kushushwa kwa vifaa vinavyohitajika viwanjani hapo.