RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu wa Taifa kuongeza wataalamu wenye uwezo wa hali ya juu, ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na magonjwa ya figo hapa nchini.Dk. Mwinyi ametoa rai hiyo katika Kongamano la nane (8) la Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Figo (NESOT), lililofanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni, Mkoa Mjini Magharibi.

Alisema kuna haja ya kuongeza wataalamu wenye uwezo wa hali ya juu katika kukabiliana na ongezeko la maradhi hayo ambapo takwimu zinabainisha magonjwa ya figo ni tatizo kubwa linaloikabili Tanzania na Dunia kwa ujumla.

Aliitaka NESOT kuwataka wanachama wake kuwa mfano bora wa kuwavutia Vijana wapya ili wahamasike kusomea na kujiunga na fani hiyo muhimu, pamoja na chama hicho kuendeleea kuwajengea uwezo watoa huduma katika Hospitali za Rufaa na Vituo vyote vya Huduma za msingi nchini.

Alisema tatizo la figo ni kubwa Duniani, wakati ambapo takwimu zinaonyesha hapa Tanzania watu saba hadi kumi kati ya watu 100 wanaougua ugonjwa huo.

Dk. Mwinyi alisema katika kukabiliana na hali hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuchukua hatua kwa kuongeza vituo vya kutoa huduma za kusafisha damu (hemodialysis) kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo; bila malipo yoyote.

“Hivi karibuni tumesogeza huduma hizi katika kisiwa cha Pemba ili ziweze kupatikana huko na kuondoa tatizo la wagonjwa hao kulazimika kufuata huduma hapa Unguja”, alisema.

Alitumia nafasi hiyo kukipongeza NESOT kwa kufadhili masomo ya Madaktari bingwa wabobezi saba (7) katika fani ya magonjwa ya Figo, sambamba na kusaidia uanzishaji wa mafunzo ya shahada ya Uzamivu (Phd) ya fani ya uuguzi wa magonjwa ya Figo yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi (MUHAS).

“Taarifa njema zaidi ni kwamba tayari mwaka huu matunda yameanza kupatikana baada ya wataalamu 10 kuhiitimu masomo yao”, alisema.

Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa Wizara ya Afya kuangalia uwezekano wa wauguzi wenye sfa kuweza kujiunga na masomo hayo ili kuongeza wataalamu hapa nchini.

Aidha, alisema pamoja na changamoto kadhaa ziliopo katika kuukabili ugonjwa huo, Tanzania imepiga hatua kwa kuanzisha huduma za Upandikizaji Figo, ambapo zaidi ya wagonjwa 80 tayari wamepata huduma hiyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Aliutaka Uongozi wa Wizara Afya Zanzibar pamoja na Viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja kutafakari kwa namna gani wanaweza kuanzisha huduma hiyo.

Dk. Mwinyi aliwataka wataalamu hao kuzingatia namna bora ya kuielimisha jamii kutambua namna ya kujikinga na ugonjwa huo huku wakiwema mazingatio katika upatikanaji wa Lishe bora, kupunguza matumizi ya chumvi na mafuta, kuepuka uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe pamoja na kudumu katika kufanya mazoezi.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alipongeza ushirikiano wa karibu uliopo kati ya wataalamu wa Tanzania Bara na wenzao wa Zanzibar, akibainisha haja ya kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha wataalamu hao kushirkiana katika tiba za magonjwa tofauti , ikiwemo Figo ili kuondokana na hali iliopo ya wagonjwa wengi kupelekewa nje ya nchi kwa matibabu.

Aidha, alisema azma ya serikali ya kuanzisha huduma za Bima ya Afya inapaswa kwenda smbamba na uboreshaji wa vitendea kazi.

Nae, Waziri wa Afya Nassor Ahmeid Mazrui alisema Wizara hiyo imeweka kipaumbele katika kusomesha wataalamu wa kada muhimu zenye upungufu mkubwa wa wataalamu, wakiwemo madaktari na wauguzi.

Alisema katika kuondokana na changamoto iliokuwa ikiwakabili wagonjwa wa Figo walioko Kiisiwani Pemba ya kufuata huduma hizo Unguja, Wizara hiyo imeweka mashine tano za kusafishia damu katika Hospitali ya Abdalla Mzee Kisiwani humo.

Aidha, alisema Wizara inalenga kuweka mashine za kusafishia damu zisizopungua kumi katika kila Hospitali ya Wilaya, pale ujenzi wake utakapokamilika, wakati ambapo Hospitali ya Mkoa ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februry mwakani, imepangiwa kuwekewa mashine 12 za aina hiyo.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau na washirika wa maendeleo pamoja na Asasi zisizo za Kiserikali kuunga mkono juhudi za Serikali na kushirikiana katika katika kutuokomeza ugonjwa huo.

Mapema, Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Figo Tanzania Dk. Onesmo Kisanga alisema kuna magonjwa kadhaa yanayochangia maradhi ya Figo, ikiwemo kifafa cha mimba, maambukizi yatokanayo na Malaria, kuumwa na Nyoka pamoja na matumizi ya dawa yasiozingatia ushauri w adaktari.

Alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya nne, kwa kuanzisha Programu ya upandikizaji wa Figo nchini, ambapo takwimu zinabainisha kuwa watu 90 tayari wamepandikizwa figo kwa uhakika tangu programu hiyo ilipoanza.

Alitoa shukrani kwa Serikali zote mbili (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) kwa kuboresha huduma za kukabiliana na maradhi hayo na kusema vituo 260 vya kusafisha damu vimeanzishwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema katika kongamano la mwaka 2018 ambalo lilifanyika Zanzibar lilipitisha Azimio la kufanyika mafunzo bobezi, jambo ambalo limefanikiwa kwa kukishirikisha Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Skuli (MUHAS), ambapo tayari wauguzi 10 wamefaulu mafunzo hay, huku wengine 15 wakiendleea na mafunzo mmoja, mmoja wao akiwa ni Mzanzibari.

Kongamano la nane la Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Figo Tanzania (NESOT) limewashirikirsha madaktari, wauguzi, washiriki wa Kikanda Tanzania,  Wawakilishi wa Wagonjwa na wadau mbali mbali wanaohughulikia magonjwa ya Figo, likifadhiliwa na taaisis na mashirika mbali mbali nchini, huku mfadhili mkuu ikiwa ni Shirika la Harsh Phamaceuticals Limited