RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali anayoiongoza tayari imepita lengo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinzi (CCM) ya kutaka zijengwe barabara za kilomita 200 Unguja na Pemba na badala yake imetekeleza kwa vitendo ujenzi wa kilomita 500 za barabara zilizojengwa nchi nzima.

Dk. Mwinyi, ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kilomita 6.5 ya Uwanja wa ndege, Kiembesamaki hadi Mmazi Moja Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema, Serikali inajenga mtandao wa barabara za kilomita 100 mijini kwa Unguja na Pemba pamoja na ujenzi wa kilomita 130 za barabara za Tunguu-Makunduchi, Kisauni - Fumba na Chake – Mkoani, Pemba mbali na barabara za kilomita 285 za vijini.

Rais Dk. Mwinyi alieleza, ujenzi wa barabara hizo zinazotegemewa kudumu kwa zaidi ya miaka 50 hadi 70 ijayo kutokana na uimara na ubora wa kiwango cha hali ya juu uliojumuishwa na miundombinu ya kupishia maji ikiwemo mitaro ya maji machafu, miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo maji safi, umeme na njia za mawasiliano pamoja na barabara za watembea kwa miguu.

Akizungumzia adha za usafiri wa umma nchini, Rais Dk. Mwinyi alieleza, Serikali imedhamiria kuondosha changamoto ya foleni barabarani na usumbufu kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara za juu Amani - Mwanakwerekwe.