RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali iko tayari kupokea msaada wa chanjo COVID -19 pamoja na misaada mbali mbali ya kitabibu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).Dk. Mwinyi amesema hayo Ieo Ikulu Jijini Zanzibar , alipokutana na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani, anaefanyia shughuli zake nchini Tanzania Dr. Tigest Ketsela Mengestu, aliefika kujitambulisha.

Amesema sekta ya Afya nchini ina mahitaji makubwa ili iweze kufanikisha lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo azma ya WHO kuendelea kuisadia Zanzibar katika nyanja mbali mbali, ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa madaktari na wafanyakazi wa Afya pamoja na uimarishaji wa miundombinu ni jambo muhimu.Alisema katika hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo Bima ya Afya nchini.

Aidha, alisema kuna haja ya kuimarisha miundo mbinu ya huduma za Afya, hususa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambayo hivi sasa haikidhi mahitaji ya wakati katika utoaji wa huduma kutokana ongezeko la watu pamoja na ufinyu wa nafasi.Alisema Hospitali hiyo yenye majengo ya kale, ina ufinyu mkubwa wa nafasi,  ikiwemo uchache wa vyumba vya upasuaji hususan kwa magonjwa makubwa kama vile moyo pamoja na kuwa na wodi chache za kulaza wagonjwa.

Alisema hali hiyo imeifanya Serikali kuweka malengo ya kujenga Hospitali kubwa na ya kisasa katika eneo la Binguni, Mkoa wa Kusini Unguja.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alilishukuru shirika hilo kwa mashirikiano pamoja na misaada mbali mbali inayotoa kwa Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Afya nchini.

Mapema, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO)  nchini Tanzania Dr. Tigest Ketsela Mengestu, alisema WHO iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala la kuimarisha sekta ya Afya nchini, hususan katika utoaji wa mafunzo kwa madaktari na wafanyakazi wa sekta hiyo.Alisema Shirika hilo linalenga kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya ili waweze kutoa elimu hiyo kwa wananchi katika kukabiliana na   magonjwa mbali mbali kama vile kipindupindu, ukosefu wa lishe, mafua makali pamoja na COVID -19.

Aidha, akaiomba Serikali kubainisha aina ya chanjo ya COVID-19 inayohitajika, sambamba na kuhakikisha mchakato wa kuwapatia chanjo Mahujaji wa Zanzibar unakamilika kwa wakati, ikizingatiwa muda mdogo uliobaki kabla ya kufanyika kwa ibada hiyo.Dr. Mengestu alimhakikisha Rais Dk. Mwinyi kuwa WHO itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya Afya nchini, ikiwa ni hatua ya kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu, ulioasisiwa tangu miaka ya 1960.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezungumza na Mwakilishi mkaazi wa ‘UN Women Tanzania’ Hodan Addou, aliefika Ikulu Jijini Zanzibar.Dk. Mwinyi amesema Serikali iko makini kuhakikisha wanawake wa Zanzibar wanapata haki zao pamoja na kuondokana na vitendo vyote vya ukandamizaji, ikiwemo udhalilishaji dhidi yao na watoto.

Aidha, alisema Serikali imekuwa ikiwateua wanawake zaidi katika nafasi mbali mbali za uongozi sio kwa upendeleo, bali kutokana na juhudi,  uwezo na uaminifu mkubwa walionao.

Nae, Mwakilishi Mkaazi wa ‘UN Women Tanzania’ Hodan Addou alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha Uwakilishi wa wanawake katika Uongozi, sambamba na juhudi zinazofanyika katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.Alisema UN Women Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wanawake wa Zanzibar wanapiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi.

Alisema ana imani kubwa kuwa sekta ya Uchumi wa Buluu italeta faida kubwa kwa wanawake, hivyo akaunga mkono juhudi za Serikali zinazoendelea kuchukuliwa kuimarisha sekta hiyo, ili kuinua hali zao kiuchumi.