RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza ushirikiano kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ili kuweza kukusanya kodi ipasavyo.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Alphayo Japan Kidata akiwa na ujumbe wake wakati walipofika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Katika maelezo yake , Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kuna haja ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kufanya kazi kwa pamoja na azma ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi hapa Zanzibar.Alieleza kuwa mashirikiano ya pamoja kati ya Taasisi hizo mbili kutaondosha changamoto zilizokuwepo hapo siku za nyuma ambapo ukusanyaji wa kodi kwa upande wa Zanzibar haukuwa ukifanyika vyema.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kufanya kazi kwa pamoja kati ya taasisi hizo mbili kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililokusudiwa na kuondosha upotezaji wa kodi sambamba na kutokuwa kikwazo katika kupatikana kodi hiyo.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa juhudi zake za makusudi inazozichukua katika ukusanyaji wa kodi hapa nchini.

Alifahamisha kwamba hata kwa upande wa Zanzibar ufanisi umekuwa mkubwa lakini hata hivyo, Rais Dk. Miwnyi alisisitzia haja ya kuimarisha ushirikiano ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa wataalamu watakaosaidia ukusanyaji wa kodi.Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba ni vyema mafanikio yaliopatikana Tanzania Bara kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) yakafanywa pia, kwa upande wa Zanzibar ili Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), iweze kufanya kazi zake ipasavyo.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila aina ya ushirikiano kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana katika suala zima la ukusanyaji wa kodi na kuahidi kwamba kwa upande wake milango yake iko wazi katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana.

Nae Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Japan Kidata alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Taasisi yake imekuwa na mashirikiano makubwa kati yake na Bodi ya Mapato Zanzbar (ZRB) na inaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha ndoto za viongozi wakuu zinafikwia.

Alieleza kwamba (TRA), imeweka mikakati kabambe katika kuhakikisha uwezo na uweledi uliopo katika Taasisi hiyo kwa upande wa Tanzania Bara pia, unafanya kazi kwa upande wa Zanzibar ili kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.Aliongeza kuwa kwa vile Taasisi hiyo ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vyema ikafanya kazi zake katika pande zote mbili.

Hivyo, Kamishna Kidata alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba atahakikisha yeye na uongozi wake wa Mamlaka hiyo ya Mapato Tanzania (TRA), wanafanya kazi kwa bidii ili kufikia ndoto za viongozi wakuu katika suala zima la ukusanyaji wa kodi hapa nchini.Kamishna Kidata alisema kuwa tayari Taasisi yake imeshaanza kuleta wataalamu hapa Zanzibar katika kuhakikisha wanatoa elimu juu ya masuala mbali mbali ya ukusanyaji wa kodi wakiwemo wataalamu wa maadili, wataalamu wa TEHAMA (ICT) pamoja na wataalamu wengine ili ukusanyaji wa kodi hapa Zanzibar uweze kwenda sawa.

Alisema kuwa si jambo la busara kuona kwamba upande mmoja wa Muungano unapata mafanikio katika ukusanyaji wa mapato na upande mwengine ukabaki na changamoto, na ndio maana wameweka mikakati ya kuhakikisha pande zote mbili katika suala la ukusanyaji wa kodi zinakwenda sawia.

“Tutaendelea kushirikiana na tunataka (ZRB) na (TRA) tuwe kitu kimoja…..mimi na timu yangu tutahakikisha ile ndoto mliyonayo viongozi wetu wakuu wa nchi inafikiwa katika suala zima la ukusanyaji wa kodi”,alisisitiza Kamishna Kidata.

Aidha, Kamishna Kidata alieleza juhudi inazozichukua (TRA) hivi sasa katika kuhakikisha inatengeneza mfumo wa kuwasaidia na kuwarahisishia wananchi kutambua kodi zao na kuzifanyia kazi kirahisi badala ya kwenda katika ofisi za Taasisi hiyo.

Sambamba na hayo, aliongeza kuwa hatua hiyo inachukuliwa na (TRA), ili kupunguza na hatimae kuondosha kabisha changamoto zinazowakabili wananchi huku akisisitiza kwamba Taasisi hiyo inaendelea kuondoa changamoto kwa wale watendaji wote wasio na maadili katika Taasisi hiyo.