Media » News and Events

Dk.Hussein Ali Mwinyi ametoa shukurani kwa Viongozi na wanachama wa Chama cha M Mapinduzi Wilaya Kaskazini ‘B’

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa shukurani za dhati kwa Viongozi na wanachama wa Chama cha M Mapinduzi Wilaya Kaskazini ‘B’ Unguja, kwa kazi kubwa waliyofanya na kukipatia ushindi chama hicho katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 2020.

Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo leo, alipozungumza na viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa CCM Mkoa Kaskazini Unguja, uliopo Mahonda.Amesema amelazimka kutoa shukrani hizo kwa wanachana na viongozi hao kutokana na kazi kubwa na nzuri waliyofanya hadi kukipatia ushindi wa kishindo chama hicho, hivyo kuthibitisha uwezo na nguvu kubwa ilizonazo kuliko wakati mwengine wowote ule.

Aidha, lisema hatua hiyo imekijengea heshima chama hicho , kwani kimeweza kupata viti vingi katika Baraza la Wawakilishi.

Mapema, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Idd Ame alisema wanachama wa CCM Mkoa huo wanaunga mkono kwa dhati juhudi za Rais Dk. Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.Alisema viongozi hao kutoka ngazi tofauti za Chama hicho walifanya kazi kubwa ya kukipatia ushindi , ikiwa pamoja na kulikomboa Jimbo la Bumbwini lilikowa mikononi mwa kambi ya upinzani.

Katika hatua nyengine, wanachama mbali mbali walipata fursa ya kutoa maoni,  ushauri pamoja na mapendekezo yao na kuiomba serikali kuwapatia akinamama wa Wilaya hiyo mikopo yenye masharti nafuu, kwa kigezo kuwa wengi wao ni wajasiriamali wanaohitaji kuendelezwa kutokana na kuwa na mitaji midogo.Wameiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa vijana wa Wilaya hiyo katika upatikanaji wa fursa za masomo, ili weweze kushiriki kikamlifu katika miradi mikubwa ya Ujenzi wa Bandari itakapoanza kutekelezwa katika eneo la Mangapwani, na hivyo kupata nafasi za ajira, kwa kuzingatia kuwa miradi hiyo imo ndani ya Wilaya hiyo.

Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayuob Mohamed Mahamoud alisema mkutano huo umeongeza matumaini na matarajio makubwa kwa wanachama wa Chama hicho Mkoani humo kwa kigezo cha kuimarika kiuchumi, kupita sekta uchumi wa Buluu, huku akiahidi uongozi wa Mkoa huo kutekeleza maagizo yote ya Chama na Serikali aliyoyatoa.

Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, ina wakaazi wapatao 81767, ambapo idadi ya wanachama wa CCM kutoka Majimbo matatu ya Uchaguzi ni 16,778.