Media » News and Events

Dk.Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair wa kuiunga mkono Zanzibar kupitia taasisi yake ya Mabadiliko Ulimwenguni.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya Mlango wa Zanzibar mgeni wake Waziri Mkuu Mstaaf wa Uingereza Mhe.Tony Blair, baada ya kumaliza mazungumzo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair wa kuiunga mkono Zanzibar kupitia taasisi yake ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change).Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mstaafu huyo wa Uingereza Tony Blair ambaye alikuwepo Zanzibar kwa ziara maalum ya siku moja.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Taasisi ya Waziri Mkuu huyo Mstaafu wa Uingereza ili kuihakikisha azma iliyokusudiwa inafikiwa.Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri huyo Mstaafu wa Uingerza kwa kufanya ziara Zanzibar na kuweza kubanilishana mawazo katika mustakabali mzima wa kuiletea maendeleo Zanzibar.

Alieleza kwamba ana matumaini makubwa kuwa mazungumzo baina yao yatakuwa chachu ya maendeleo hasa ikizingatiwa kwamba Tony Blair ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi duniani.Hivyo Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani zake kwa Waziri Mkuu huyo Mstafu na kueleza kwamba nia yake njema ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Taasisi yake ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change) itaweza kuleta manufaa makubwa ya kimaendeleo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri Mkuu huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kutekeleza mikakati, mipango na dira zilizowekwa na Serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kuiletea Zanzibar maendeleo endelevu.

Nae Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Taasisi yake iko tayari kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika kutafuta njia bora za kupanga mikakati ya kutekeleza mipango ya maendeleo.Tony Balair alieleza kwamba timu yake kutoka Taasisi anayoiongoza iko tayari kuja na kukaa na wataalamu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuanza taratibu hizo za kuhakikisha utekelezaji wa mazungumzo hayo unafanyika ikiwa ni pamoja na kusaidia vipaumbele vya Serikali.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu alisema kuwa Taasisi yake inathamini sana juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Hussein Mwinyi na kuahidi kwamba itakuwa bega kwa bega katika kuhakikisha inashiriki ipasavyo kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.Katika mazungumzo hayo, Tony Blair alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Taasisi yake imekuwa ikifanya kazi katika nchi mbali mbali katika Bara la Afrika hivyo, kushirikiana na kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutaweza kupanua wigo wa maendeleo.

Sambamba na hayo, Waziri Mkuu huyo Mstaafu aliyasifu mazingira mazuri ya Zanzibar na kuahidi kurudi tena kuja kuitembelea zaidi Zanzibar mara baada ya kumazika kwa janga la maradhi ya COVID 19 duniani ambalo limemnyima fursa ya kutekeleza azma yake hiyo kwa hivi sasa.