RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kuanzishwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ni miongoni mwa mikakati ya kuirejesha Zanzibar katika uasili wake wa kuwa na Taasisi hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya kuitembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo iliyopo Langoni, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kujionea hatua za uendelezaji wa majengo ya Taasisi hiyo ambayo ni miongoni mwa Taasisi tatu mpya zilizoanzishwa hivi karibuni katika uongozi wake.Rais Dk. Shein alieleza kuwa historia inaonesha kuwa Zanzibar ni ya mwanzo katika Afrika ya Mashariki kuwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ambapo pia uanzishwaji wa Kituo hicho kwa mara nyengine tena ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo lengo lake kuu ni kufanya utafiti wa mifugo kwa kiwango cha juu.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alieleza kuwa eneo hilo lenye heka 26 kuliwacha bila ya kulifanyia kazi si jambo la busara kwani ni eneo lenye sifa zote katika masuala ya kilimo, ufugaji pamoja na masuala ya utafiti.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dk. Kassim Gharib Juma kwa kuanza na hatua nzuri na kueleza matumaini yake makubwa baada ya miaka miwili ya Taasisi hiyo itakavyokuwa.Aidha, Rais Dk. Shein aliuahidi uongozi wa Taasisi hiyo kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha TZS Bilioni 1.2 zinapatikana katika kuhakikisha Taasisi hiyo inaendelezwa na kuimarika zaidi.
Alieleza kuwa eneo hilo ambalo mwanzo lilikuwa likitumiwa na Kampuni ya ZAPOCO, kwa ajili ya kufuga kuku tayari hivi sasa Serikali imeshamalizana na Kampuni hiyo na limerejeshwa kwa Serikali na uwamuzi uliochukuliwa ni kujengwa Taasisi ya Mifugo ambayo ujenzi wake unandelea.“Tuliwarudi fedha kwa ajili ya eneo hili, fedha ambazo ni kwa ajili ya kulipa miundombinu ya Kampuni hiyo na sio ardhi kwani ardhi ni ya Serikali”,alisisistiza Dk. Shein.
Mapema Rais Dk. Shein alipata maelezo juu ya ujenzi mpya eneo la Utawala unaoendelea wa Taasisi hiyo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Dk. Kassim Gharib Juma na baadae kutembelea mabanda ambayo yanatayarishwa kwa ajili ya utafiti zikiwemo tafiti kwa ajili ya ngombe, kuku, mbuzi, kondoo, kuku pamoja na mwani.Pia, Rais Dk. Shein lipata fursa ya kujionea hatua za awali zilizoanza kuchukuliwa na Taasisi hiyo kwa ajili ya utafiti ambapo tayari imeshaanza kupokea wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali duniani wanaofanya tafiti katika eneo hilo na kukutana na mwanafunzi Leanna Kelly kutoka Chuo Kikuu cha California nchini Marekani akishirikiana na wataalamu wazalendo akiwemo Faki Ame Kesi na wengineo.
Pia, wataalamu hao walieleza namna wanavyofanya utafiti wa kuangalia ubora wa chakula cha kuku na hivi sasa wamo katika mchakato wa kuangalia aina bora ya chakula na tayari wameanza kwa kuku wa kisasa (broiler).
Nae Dk. Waridi Abdalla Mussa alieleza jinsi hatua za awali wanazozichukua katika kukusanya kuku wa kienyeji kwa ajili ya kuwafanyia utafiti pamoja na kueleza namna ya utafiti wa ngombe wa kienyeji walioufanya na kugundua maradhi ya kichocho na minyoo katika Wilaya zote za Unguja na Pemba huku akieleza namna ya wanavyokabiliana na maradhi.Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alifanya ziara ya kutembelea eneo la Binguni Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja ambalo linatarajiwa kujengwa Hospitali mpya ya Rufaa pamoja na kusomeshea Madaktari na eneo la Taasisi ya Utafiti wa Afya.
Mapema Rais Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Afya na baadae alipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi kupitia kwa Katibu wa Kamisheni ya Ardhi Hemed Rashid na viongozi wengine wa Wizara hiyo na kueleza jinsi hatua zilizochukuliwa katika kulipima eneo hilo kama walivyopata maekelezo kutoka kwa Rais.Aidha, uongozi huo ulieleza namna eneo hilo litakavyowafaidisha wananchi wakiwemo vijana wajasiriamali pamoja na Serikali katika kulifanyia shughuli mbali mbali zilizopangwa.
Akiwa katika eneo hilo, Rais Dk. Shein alipata fursa ya kulitembelea na kuangalia mipaka yake mara baada ya kupata maelezo hayo kutoka kwa viongozi hao ambapo alitembea kwa miguu zaidi ya kilomita mbili na nusu ili kujionea mwenyewe mipaka ya eneo hilo lote.Akiwahutubia wananchi na viongozi mbali mbali wa chama na Serikali waliofika katika eneo hilo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa hakuna mwananchi hata mmoja atakaefukuzwa katika eneo hilo ila kwa wale waliokuwemo ndani ya eneo hilo tarajiwa watafanyiwa taratibu nyengine za makaazi.
Aliongeza kuwa Hospitali inayotaka kujengwa katika eneo hilo ni ya Wananchi wote wa Zanzibar hivyo kila mmoja anapaswa kujua kuwa eneo hilo linamgusa huku akiwahakikishia wananchi kuwa Hospitali katika eneo hilo itajengwa kwani mchakato wa kupata fedha tayari umeshakamilika.
Dk. Shein alisema kuwa eneo hilo ambalo ni la Serikali lina zaidi ya hekta 53 ambalo lilikuwa la uwanja wa ndege wa mwanzo kabla ya kuhamishiwa Kisauni lilikatwa na kupimwa sivyo ndivyo na tayari ameshatoa maelekezo kwa Wizara ya Ardhi, Wizara ya Afya, Ofisi ya Mkoa, Wilaya, Halmashari pamoja na Masheha kukaa pamoja ili kuliweka alama upya za mipaka.Alisema kuwa katika eneo hilo ambalo walijitokeza baadhi ya watu waliowatapeli taasisi ya ‘African Muslim Agency’ ambapo taaasisi hiyo ilijenga majengo katika eneo hilo bila ya kufuata taratibu za Serikali, bila ya kuwa na kibali, hati na taratibu zote za ujenzi.
Rais Dk. Shein aliongeza kuwa kutokana na taasisi hiyo kuwa na malengo na madhumuni mazuri Serikali imeamua kuwapa eneo jengine kwa ajili ya ujenzi wanaokusudia pamoja na kuwapa fedha za kuwasaidia kuendelea na ujenzi wao mwengine ambazo si kwa ajili ya fidia.Alisema kuwa tayari majengo hayo yameshakabidhiwa kwa Wizara ya Afya ambapo Wizara hiyo inatarajia kujenga Taasisi ya Afya ambapo wanafunzi wote wanaosoma masuala ya afya watahamishiwa katika eneo hilo ambapo pia, eneo hilo litajengwa nyumba za wafanyakazi.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kufanya ziara hiyo muhimu ya kutembela katika maeneo hayo yote.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdala Juma Mabodi alieleza kuwa azma ya ujenzi wa Hospitali katika eneo hilo alikuwa nayo Rais Dk. Shein tokea akiwa mtumishi wa Wizara ya Afya ambapo yeye mwenyewe wakati huo akiwa Mkurugenzi.Alisisitiza kuwa mambo yote hayo anayoyafanya Rais Dk. Shein ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 huku akitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuonesha uongozi shirikishi kwa kuwashirikisha viongozi wote wa CCM na Serikali katika ziara hiyo ambayo ni moja ya ziara za utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.