MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi ameinasihi jamii kuendeleza mema yote ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hata baada ya kumalizika kwa ibada za mfungo huo.Mama Mariam aliyasema hayo, kwenye ziara yake ya kuwatembelea wazee, watoto yatima na jamii zenye uhitaji katika vituo mbalimbali vilivyopo ndani ya Wilaya tatu za Unguja kwa lengo la kuwafariji na kuwapa mkono wa Iddi pia kujumuika nao pamoja wakati wa furaha za siku kuu za Eid el Fitri.

Mama Mariam Mwinyi pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), alitumia fursa ya kuzungumza na watoto yatima wa vituo vya kulelewa watoto hao vilivyopo Fuoni Mambo sasa, Wilaya ya Magharibi A, Kijiji cha kulelea watoto yatima SOS, Mombasa - Wilaya ya Magharibi B pamoja na nyumba ya kuwatunzia watoto hao iliopo Mazizini Mkoa wa Mjini Mkoa wa Mjini Magaharibi.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi aliwaasa watoto hao kuendeleza tabia njema kwa kuendeleza ibada na mazuri yote wanayoelekezwa wa wakubwa wao.Sambamba na kuwashukuru walezi na walimu wanaowasimamia watoto hao kwa juhudi za kuwakuza vyema.“Nafarajika sana kipindi hiki cha siku kuu nikiwa pamoja nanyi, kadri ninavyowaona mnafurahi nami siku kuu yangu huanzia hapo, furaha yangu mimi ni kukuoneni mkiwa na furaha siku zote” alizungumza kwa hisia Mama Maiam Mwinyi.

Akizungumza kwenye ziara hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma, alisifu na kupongeza ziara za Mama Mariam Mwinyi kwa wazee na watoto hao na kueleza kuwa ziara hizo ni utaratibu aliojiwekea Mama Mwinyi kila ifikapo Mwenzi Mrukufu wa Ramadhani pamoja na siku kuu kuwatembela na kufurahika nao.

Kwa upande wa wazee na watoto hao walimshkuru Mama Mariam Mwinyi kwa Sadaka ya futari aliyowapatia kipindi cha Ramadhani pamoja na kujumuika nao wakati huu wa furaha ya siku kuu ya Eid el Fitri.Pia Wazee hao walitumia fursa hiyo kumpa pole Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa msiba wa baba yake mzazi, Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliefariki dunia Febuari 29 mwaka huu.

Vile vile wazee hao walisifu ushirikiano wanaoupata kutoka Wizara Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kuendelea kuwa karibu nao wakati wote, pia wazee hao walimtakia heri Rais Dk. Mwinyi nakumuombea neema kwenye majukumu yake ya kuiongoza Zanzibar.Bi. Tatu Rajab Juma, mzee wa kituo cha Sebleni kwa niaba ya wazee wenziwe alisifu jitihada za Mama Mariam Mwinyi pamoja na Rais Dk. Mwinyi kwa kuendelea kuwaenzi, kuwatunza na kuwathamini.

Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Suzan Peter Kunambi kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mjini na Magharibi B, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah na Khatib Mwadini Khatib pamoja na maofisa mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar