Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi leo Agosti 16, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman aliyemaliza muda wa uwakilishi nchini Tanzania Mhe. Ali Bin Abdallah Bin Salim Al Mahrooq, Ikulu Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Al Mahrooq alitumia fursa hiyo kumuaga rasmi Rais. Dk. Mwinyi huku akisisitiza kuendelezwa ushirikiano uliopo hususani katika sekta za kibiashara baina ya Oman na Zanzibar.

Aidha Balozi Al Mahrooq ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Oman wakati wa muda wake hapa nchini kwenye maendeleo mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa sekta ya Elimu Zanzibar, kukarabati majengo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar na miradi mingi ya maendeleo.

Kwa Upande wake Rais. Dk Mwinyi amemshukuru Balozi Al Mahrooq na kuishukuru Oman kwa ushirikiano mkubwa na kumtaka afikishe salam kwa Sultan wa Oman, Mhe. Haitham Bin Tariq Al Said kumueleza Zanzibar iko tayari na itaendelea kushirikiana na Oman katika sekta mbalimbali za kibiashara na kijamii kwani Oman na Zanzibar zina historia kubwa na ya kipekee.