Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itachukua hatua kuhakikisha watu waliolipwa fidia zisizostahiki katika maeneo yaliyopitishwa miradi ya maendeleo wanazirejesha fedha hizo Serikalini.
Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa ripoti iliyowasilishwa na Tume ya Tathmini ya Masuala ya Fidia kwa Wananchi Waliopisha Miradi ya Maendeleo imeonesha kuwa wapo baadhi ya wananchi waliolipwa fidia ili kupisha miradi lakini hawakuondoka katika maeneo hayo, huku wengine wakiendelea na ujenzi licha ya kulipwa fidia zao.
Aidha, amebainisha kuwepo kwa watu wasiostahiki waliolipwa fidia baada ya kushirikiana na baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi, na kwamba wapo waliolipwa kinyume cha sheria baada ya kuvamia maeneo yasiyo yao kisheria kwa kujenga katika hifadhi ya barabara.
Dkt. Mwinyi amesifu kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Tathmini ya Masuala ya Fidia, ambayo kwa kiasi kikubwa imegundua makosa mengi na kuisaidia Serikali kubaini watu waliolipwa fedha za ziada kwa njia ya udanganyifu kwa kushirikiana na watendaji wa sekta ya ardhi.
Amesema pia wapo wananchi wanaostahiki kulipwa lakini bado hawajapata haki yao, huku akisisitiza kuwa Serikali itachukua hatua kali za kisheria ili kurejesha fedha hizo. Aidha, amewahakikishia wananchi wanaostahiki kulipwa fidia kuwa kila mmoja atapata haki yake kwa mujibu wa sheria.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Mei 2026, alipozungumza na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Magharibi Kichama katika mkutano maalum wa kutoa shukrani baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Piccadilly uliopo Kombeni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Mwinyi, amehitimisha ziara yake ya kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM katika mikoa ya kichama ya Unguja, ikiwemo Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Magharibi.
Ziara hiyo inatarajiwa kuendelea Kisiwani Pemba katika mikoa ya Kaskazini na Kusini tarehe 13 Mei 2026.