Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa suala la kudumisha amani ni jukumu la kila Mwananchi anayependa maendeleo.Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 18 Oktoba 2025, alipojumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa na Dua Maalum ya kuiombea nchi pamoja na Uchaguzi Mkuu, hafla iliyofanyika katika Msikiti wa Muembe Shauri, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameeleza kuwa suala la kudumisha amani si la mtu mmoja pekee, bali kila Mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha amani inadumishwa katika nafasi yake.Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya kuleta umoja na maendeleo katika nyanja zote, hivyo jamii inapaswa kuweka mkazo zaidi katika kuhubiri amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki ambapo zimebaki siku chache kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali yametokana na kuwepo kwa amani kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, hali iliyoiwezesha Serikali kutekeleza mipango yake kikamilifu.Vilevile, amekumbusha kuwa vitendo au kauli za mtu vinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani iliyopo, hivyo ni vema kila mmoja akachunga maneno yake ili kudumisha amani.

Amebainisha kuwa vurugu katika nchi haziwezi kuanza kwa bunduki, bali kwa matendo au kauli ndogo ndogo ambazo baadaye husababisha uvunjifu wa amani. Amehimiza kila mwananchi kuchunga kauli zake na matendo yake ili kuendelea kulinda amani ya nchi.Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza wananchi kuendeleza utulivu uliopo sasa, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi, huku akiwataka kufuata maelekezo yote ya uchaguzi siku ya kupiga kura ili demokrasia ichukue nafasi yake.