RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja na kusisitiza kuishi kwa upendo, umoja amani na utulivu ili Zanzibar izidi kupata neema na maendeleo.Hafla hiyo ya futari imeandaliwa na Alhaj Dk. Shein kwa ajili ya wananchi wa Mkoa huo wa Kusini Unguja ilifanyika katika viwanja vya Ofisi ya Uhamiaji huko Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini, vyama vya siasa, Serikali pamoja na wananchi wa Mkoa huo.

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nae aliungana na wananchi wa Mkoa huo katika hafla hiyo ya futari akiwa pamoja na viongozi wanawake wa Kitaifa na wananchi wengine wa Mkoa huo.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Rais Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa huo Hassan Khatib alieleza kuwa amani, umoja, utulivu na mshikamano ndio falsafa pekee inayoendelea kuimarishwa katika mkoa huo kwa azma ya kujiletea maendeleo endelevu.Alieleza kuwa mafanikio makubwa yataendelea kupatikana katika Mkoa huo kutokana na amani iliyopo na kuwataka wananchi kuendelea kuisimamia kwa nguvu zao zote.

Aidha, aliwapongeza wananchi na waalikwa wote waliohudhuria katika futari hiyo maalum aliyowaandalia jambo ambalo limempa faraja kubwa na kuahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa Mkoa huo amoja na mikoa yote ya Zanzibar.

Nao wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wakitoa neno la shukurani kwa Alhaj Dk. Shein kwa futari nzuri aliyowaandalia wananchi hao.

Leo Rais Dk. Shein anatarajiwa kufutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja huko katika viwanja vya Ikuku ndogo Mkokotoni.