RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein ametoa muda wa siku saba kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kumpa taarifa juu ya ujenzi unaofanyika katika kiwanja cha Wizara ya Afya bila ya ruhusa ya Serikali huko Binguni, Wilaya ya Kati Unguja.
Dk. Shein alitoa agizo hilo katika majumuisho aliyoyatoa mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili katika Mkoa wa Kusini Unguja huko katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa kinachofahamika ni kuwa kiwanja hicho ni cha Serikali kupitia Wizara yake ya Afya ambacho kilitengwa maalum na tayari hatua za makabidhiano kati ya Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira na Wizara ya Afya imefanyika.
Akionesha kusikitishwa na hali hiyo, Dk. Shein alieleza tayari ameshamuagiza Waziri husika wa Ardhi kusimamisha ujenzi huo ili kupitisha hatua za kujua taratibu gani zimetumika hadi kiwanja hicho kuwa na majengo mengine yanayoendelea kujengwa bila ya Serikali kuwa na taarifa ya kina.
Hivyo, Dk. Shein ametoa agizo hilo na kutaka kupewa taarifa ndani ya wiki moja juu ya ujenzi huo huku akieleza kuwa katika hatua hiyo asije kuonewa mtu huku akisisitiza kuwa mizozo mingi ya ardhi hutokea kutokana na tamaa za baadhi ya watu.
Dk. Shein aliwaeleza wananchi na viongozi waliohudhuria katika majumuisho hayo kuwa ataendelea kuitetea ardhi ya Zanzibar kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wageni na wahusika wengine wa sekta ya utalii juu ya baadhi ya Polisi kuwasumbua watalii kwa kuwasimamisha mara kwa mara wakidai vibali na mambo mengine.
Hivyo, alieleza kuwa ni vyema uongozi wa Mkoa ukashirikiana na Jeshi la Polisi katika kulitizama suala hilo na kuona kwamba hatua zinazochukuliwa na Mkoa za kuimarisha ulinzi haziathiri sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar.
Pia,aliuagiza uongozi wa Mkoa kuchukua hatua kali katika kuifanyia kazi changamoto waliyoieleza kwenye taarifa yao kwamba wapo wananchi wenye kukodisha nyumba zisizosajiliwa kisheria hali ambayo inakosesha mapato na ni hatari kwa usalama na utamaduni wa Zanzibar huku akiwataka wananchi kupiga vita Ukimwi na maambukizi yake.
Dk. Shein alieleza haja ya Kamati ya Ulinzi ya Usalama ya Mkoa kuandaa mikakati na kuchukua hatua za kukabiliana na kukomesha vitendo vya magendo katika Mkoa huo hasa katika maeneo ya kisiwa cha Uzi.
Katika suala la mabadiliko ya tabianchi Dk. Shein alitaka Mkoa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kuandaa mikakati imara ya kukabiliana na athari za ongezeko la kina cha maji ya bahari na mmongonyoko wa ardrhi katika fukwe.
Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika kuwashajiisha wawekezaji wa mahoteli kujenga ngome na kuta katika maeneeo wanayowekeza yaliyo katika fukwe badala ya kukaa na kusubiri Serikali kufanya hivyo.
Sambamba na hayo, aliupongeza Mkoa kwa hatua ulizozichukua katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa katika Mkoa katika nyakati mbali mbali lakini alisema baadhi ya maagizo hayo hayajafanyiwa kazi vizuri likiwemo suala la utoro wa watoto skuli.
Alieleza kuwa kiwango kilichopungua cha asilimia 0.4 ni kidogo sana, takwimu zinazoonesha bado watoto wanatoroka.
Pamoja na hayo,Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Mkoa wa Kusini kwa kujitolea katika kushirikiana na viongozi wao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zao zinazowakabili katika maeneo yao.
Akieleza kuhusu miradi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Shein aliupongeza Mkoa huo kwa mwammko wao wa ujenzi wa Matawi ya kisasa ya chama hicho na kueleza kuwa hatua hiyo itaendelea kukiwekea heshima zaidi chama chao na kuwafanya watumishi wake kufanya kazi katika mazingira yalio bora zaidi.
Alipongeza juhudi za kilimo zinazoendelezwa katika maeneo mbali mbali kikiwemo kilimo cha ndimu huko Ukongoroni pamoja na kilimo cha mboga huko Paje Mtule na kueleza azma ya Serikali katika kuwasaidia wakulima pamoja na wanaushirika waliojikusanya katika vikundi vyao ama ushirika.
Aidha, Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Mkoa kwa hatua uliyoifikia katika utekelezaji wa mpango wa upelekaji wa Madaraka kwa wananchi ambao unajulikana kwa jila la ‘ugatuzi’ na kueleza kutiwa moyo na Mkoa huo ambao tayari umeshaanza kutekeleza mpango huo tokea Julai mwaka huu wa 2017.