Media » News and Events

Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewapa pole wananchi wote walioathiriwa na mvua za vuli zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewapa pole wananchi wote walioathiriwa na mvua za vuli zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.Al hajj Dk. Mwinyi alisema, kipindi hiki cha msimu wa mvua kwabahati mbaya yapo baadhi ya maeneo watu wamepata maafa makubwa yaliyotokana na mvua hizo.

Rais Al hajj Dk. Mwinyi ameyasema hayo Masjid Al - Kheiry Nyamanzi, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi alipojumuika pamoja na waumini wa Kiislamu kwenye Ibada ya Sala ya Ijumaa.Al hajj Dk. Mwinyi, alitumia fursa hiyo, kuwapa pole wananchi wote waliopata maafa kwa mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kutupa mvua zenye heri zisizokuwa na maafa.

“Nawapa pole ndugu zetu wote waliopata maafa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ni wajibu wetu sote kumuomba Mwenyezi Mungu atupe mvua zenye neema, atuepushie mvua zenye maafa” kwahisia alizungumza Al hajj Rais Dk. Mwinyi.Pia, Al hajj Dk. Mwinyi, aliendelea kuhimiza suala la amani, umoja na mshikamo kwenye jamii na kusisitiza kuwa ni jambo la msingi katika ustawi wa nchi na watu wake katika kukuza maendeleo na kujenga uchumi endelevu.

Alsema, ataendelea kusisitiza suala la kudumisha amani ya nchi kwani ni jambo la msingi na la kwanza kwa taifa lolote.Aliongeza, kukosekana kwa amani ya nchi hakutokua na maendeleo yoyote wala ustawi wa nchi na watu wake kila kitu kitaharibika.“Suala la amani lazima tulirudie mara kwa mara kwa sababu lina umuhimu mkubwa katika nchi, kwa hivyo, ndugu zangu tuendelee kuhimizana kuhusu amani, juu ya umoja wa watu na mshikamano ili mambo mengine yaendelee kustawi kwajili ya maendelo ya taifa letu” alilisitiza Al Hajj Dk. Mwinyi.

Naye, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alizungumzia umuhimu wa kufanya mema na kuacha mabaya yanayomchukiza Allah (S.W) kwa lengo la kulipwa mema kesho, Akhera.“Wanaofanya mema, Mwenyezi Mungu atawalipa mema yao na ziada na wanaofanya ubaya watalipwa kulingana na matendo yao maovu siku ya kiama” alisisitiza, Sheikh Khalid.

Akihutubu kwenye sala hiyo, Khatib Sheikh, Hafidh Ramadhan Simai, aliwanasihi waumini wa Kiislamu, kuendeleza mema na kuacha kudhulumiana kwani siku ya kiama ni nzito mno.Aliwatanabahisha waumini hao kwamba, siku ya Kiama hakutokua na malipo kutoka kwa waja waliodhulumiana bali hukumu nzito za Mwenyezi Mungu (S.W) hakimu wa haki, hivyo aliwaasa kufikiria zaidi siku ya kiama kwa kujiandaa na hukumu njema kwa Allah (S.W)