Media » News and Events

Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inafarijika kuona taasisi zisizo za Kiserikali zinasaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma mbali mbali za kijamii

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Balozi wa Shirikisho la Somali Nchini Tanzania Mhe. Zahra Ali Hassan, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha 23-11-2022, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inafarijika kuona taasisi zisizo za Kiserikali zinasaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma mbali mbali za kijamii, ikiwemo Afya na Elimu.Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na Uongozi wa Taasisi ya ‘Mwanamke Intiative Foundation’, uliofika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema Serikali inafarijika pale inapotokea taasisi iisiyo ya Kiserikali kuunga mkono juhudi za Serikali katika masuala mbali mbali, ikiwemo uimarishaji wa sekta za elimu na Afya, kwa kuzingatia kuwa haina uwezo wa kufanya kila kitu.

Alisema Serikali iko tayari kushirikiana na wadau mbali mbali wa elimu ili kufanikisha dhamira ya kuimarisha sekta hiyo, na akatumia fura hiyo kubainisha maeneo matano ambayo yamepewa kipaumbele.

Alieleza kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika uimarishaji wa miundo mbinu kwa kuanzisha ujenzi wa skuli mpya , kukarabati skuli za zamani pamoja na madarasa ya zamani pamoja na kujenga maabara na maktaba.

Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni uimarishaji wa rasilimali watu katika kada ya ualimu, kwa kuzingatia uwepo wa walimu wachache wenye kiwango kidogo cha elimu, hususan katika masomo ya sayansi.

Alisema Serikali inalenga kuongeza nguvu katika upatikanaji wa nyenzo mbali mbali, ikiwemo madawati pamoja na vitabu.

Aidha, Dk. Mwinyi Mmwinyi alisema kipambele kingine cha Serikali katika uimarishaji w asekta ya elimu ni uimarishaji wa kada ya ICT , akibainisha umuhimu wa kuwafunza mapema wanafunzi matumizi ya mifumo ya Teknolojia; ili waweze kwenda sambamba na mahitaji ya Dunia.

Dk. Mwinyi alisema uendelezaji wa Sekta ya Elimu unategemea zaidi Bajeti ya Serikali kwa asilimia mia moja na kusema fedha hizo haziwezi kutosheleza mahitaji, hivyo akabainisha azma ya Serikali ya kutafuta njia mbadala za kuongeza fedha.

Alisema Serikali kupitia Wizara Elimu iko tayari kukutana na kushirikiana na Taasisi za ‘Planet One’ ili kuona namna itakavyosaidia sekta hiyo, sambamba na Taasisi ya ‘G.S Group’  inayoshughulikia masula ya ICT. 

Dk. Mwinyi aliishukuru Taasisi ya ‘Mwanamke Initiative Foundation’ kwa Programu iliyoianzisha katika Mkoa wa Kusini Unguja inayolenga kuongeza Ufaulu kwa wanafunzi wa Mkoa huo katika Mitihani yao ya Taifa, akisema imeanza kuleta matokeo chanya.

Aidha, alitilia mkazo umuhimu wa kuelekeza nguvu katika uimarishaji wa Vyuo vya Amali, kwa kigezo kuwa kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaoanza katika ngazi za msingi, idadi inayopungua kadri kiwango cha elimu kinavyoongezeka na kuwaacha vijana wengi wakishindwa kutumia fursa mbali mbali katika soko la Ajira.

Nae, Mwenyekiti wa Taasisi ya ‘Mwanamke Initiative Foundation’ Wanu Hafidh Ameir pamoja na mambo mengine, alisema taasisi hiyo imekuwa katika juhudi kubwa za kuinga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uimarishaji wa sekta za Afya, Elimi pamoja na Kilimo.

Alisema miongoni mwa Programu iliyoanzishwa na taasisi hiyo ni ile ya kutokomeza Sufuri (division O) kwa skuli za Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo wanafunzi na walimu kutoka skuli 32 z wamepatiwa mafunzo, kupatiwa vitabu pamoja na wengine kupata udhamini katika vyuo vya Amali Tanzania Bara katika masomo ya umeme, ushoni.

Alisema katika juhudi za kuunga mkono juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya elimu, Taasisi hiyo imefanikiwa kupata taasisi tofauti kutoka mataifa mbali mbali ikiwemo Planet One kutoka Dubai pamoja na G.S. Group kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu kupitia nyanja mbali mbali.

Wakati huo huo; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezungumza Balozi wa Shirikisho la Somali nchini Tanzania, Ikulu Zanzibar aliefika kwa ajili ya kujitambulisha.

Dk. Mwinyi amewaomba wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Somalia kuja Zanzibar kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbali mbali, ikiwemo uanzishaji wa Nyumba za makaazi.

Alisema Zanzibar ina fursa nyingi za Uwekezaji, huku akibainisha miradi ya uanzishaji wa nyumba za makaazi kuwa ni eneo lenye fursa pana kwa ajili ya kuwekeza.

Aidha, alipongeza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Somalia na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ambapo wananchi wa nchi hizo wamekuwa na maingiliano ya muda mrefu pamoja na kushirikiana katika nyanja mbali mbali za kijamii pamoja na kibiashara.

Nae, Balozi wa Shirikisho la Somalia nchi Tanzania Zahra Ali Hassan alishukuru mashirikiano makubwa yaliopo kati ya wananchi wa nchi mbili hizo, huku akibainisha azma ya wananchi wa Somali kuendeleza ushirikiano huo kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali pamoja na kuimarisha biashara