Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Bi. Inger Andersen, pamoja na ujumbe wake, leo tarehe 17 Juni 2026, katika Hoteli ya Sarova Whitesands, jijini Mombasa, Kenya.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda rasilimali za bahari na kuendeleza matumizi endelevu ya rasilimali hizo kwa manufaa ya wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru UNEP kwa ushirikiano na mchango wake katika utekelezaji wa programu mbalimbali za mazingira, huku akisisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na Shirika hilo katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira, Uchumi wa Buluu na maendeleo endelevu.
