RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuhamasisha kilimo pamoja na kuunga mkono sekta ya Viwanda kwa kutambua kuwa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.Dk. Mwinyi amesema hayo alipozungumza na washiriki wa Mkutano wa 32 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wachakataji Nafaka (IAOM) uliofanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni, Mkoa Mjini Magharibi.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya kila juhudi kuhakikisha inaimarishaji uzalishaji wa mazao ya kilimo, ikizingatiwa kuwa sekta hiyo ina mchango muhimu katika kuwahakikishia wananchi usalama wa chakula.Alieleza kuwa mazao ya kilimo yana umuhimu mkubwa katika uimarishaji na uendelezaji wa Viwanda kwani mazao hayo ndio yanayotumika kama rasilimali za viwandani.
Dk. Mwinyi alisema Dunia inakabiliwa na changamaoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo kwa kiasi kikubwa inaathiri uzalishaji wa chakula, wakati huu dunia ikipita katika wakati mgumu kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukrane.Alisema nchi za Urusi na Ukrane ndio wasambaji wakubwa wa mazao ya mafuta, zao la ngano pamoja na mbolea, hivyo vita vinavyoendelea vinaathiri mnyonyoro wa usambazaji wa chakula katika maeneo mbali mbali duniani, huku hali hiyo ikichangia upandaji wa bei ya mbolea.
Dk. Mwinyi alisema mkutano huo umekuja kwa wakati muafaka kwa kuamini kuwa huenda ukasaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya chakula nchini.Aliwataka wajumbe kujadili pamoja na kuja na mipango itakayobainisha namna ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza gharama pamoja na kuongeza uhifadhi wa chakula, sambamba na kuimarisha teknolojia katika sekta hiyo.
Aidha, akatumia fursa hiyo kuwataka Wajumbe kuangalia fursa mbali mbali mbali katika sekta mbali mbali zinazopatikana Zanzibar na kuja kuwekeza.Alisema Zanzibar inatafuta wawekezaji walio tayari kufanyakazi na Serikali katika utekelezaji wa sera yake ya Uchumi wa Buluu, inayohusisha masuala ya uvuvi, mafuta na gesi, utalii pamoja na usafiri wa majini.
Nae, Waziri wa Biashara, maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaaban alisema kuwa mkutano huo umekuja kwa wakati muafaka, wakati ambapo serikali imejikita katika kutenegeneza fursa na kuimarisha mazingira ya Uwekezaji.
Mapema, Mkurugenzi Mwendeshaji wa ‘Bakhresa Grain Milling’ Mounir Bakharesa aliishukuru Serikali kwa mashirikiano makubwa inayotoa, huku akibainisha faida kubwa itakayopatikana kwa vile mkutano huo unakwenda sambamba na utekelezaji wa mikakati ya Serikali, wakati huu Dunia ikakabiliwa na changamoto kubwaya chakula.
Mkutano wa 32 wa mwaka ‘MIDEAST AND AFRIKA CONFRENCE AND EXPO IAOM, umehudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa mbali mbali wakiwemo wasambazaji wa vyakula, ambapo unajadili hali ya mdororo wa uzalishaji wa chakula pamoja na changamoto zinazojitokeza Duniani.