RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uchumi wa Zanzibar umeimarika kwa nchi kuendelea kuwa ya amani, umoja na utulivu wa watu wake.Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akisalimiana na wananchi na waumi wa msikiti wa Ijumaa, Masjid Nuru Muhammad kwa Mchina mwanzo Wilaya ya Mjini Unguja, alikojumuika pamoja nao wakati wa Sala ya Ijumaa.

Al hajj Mwinyi alisema kipindi kifupi kilichopita, Zanzibar ilipitia misukosuko ya kuyumba kwa uchumi wake muda mchache alipoingia Madarakani mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya nane mwezi Novemba mwaka 2021.Alisema, wakati huo dunia ikipitia kwenye mtikisiko mkubwa wa athari za ugonjwa wa COVID 19, hali ulioathiri zaidi uchimi wa Zanzibar, hata hivyo Dk. Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwamba sasa uchumi wa nchi yao unaendea kukua na kunawiri vizuri kadri ya amani na utulivu unavyozidi kutengemaa.

“Tulipita kipindi kigumu, sasa hivi Alhamdullillah mwanga wa wepesi unaonekana, wakati tunaingia madarakani ilikua katikati ya ugojwa wa COVID 19, mwezi ule hata mishahara ilikua shida kupatikana, hali iliendelea kwasababu ugonjwa ule uliathiri zaidi uchumi wa Zanzibar, lakini sasa kidogo kidogo hali inaendelea kukaa sawa kwa uchumi wetu kukuwa” Dk. Mwinyi aliwaeleza wananchi hao. Alisema kukua kwa uchumi, kunaipa uwezo Serikali kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo, licha ya changamoto kadhaa za uchumi zinazoendelea kuisumbua dunia kutokana na mfumko wa bei za bidhaa.

Alisema, licha ya kutengemaa kwa baadhi ya sekta za maendeleo nchini, Dk. Mwinyi alieleza bado kuna changamoto zinazosababishwa na mfumko wa bei za bidhaa ulioiathiri dunia kukutokana na kupanda kwa gharama za maisha zilizochangiwa na kupanda kwa uchumi wa dunia uliosababishwa na mambo mbalimbali.“Bado changamoto zipo sikwamba zimekwisha, sababu dunia bado haijatulia, licha ya gonjwa la UVIKO kupungua, lakini bado kunachangamoto nyengine za kidunia zinaufanya mfumko wa bei za bidhaa mbalimbali kuwa mkubwa, hivi sasa tunashuhudia bidhaa zimepanda bei kwasababu ya hali ya kidunia inavyokwenda” Alieleza Al hajj Mwinyi.

Alisema matarajio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba hali hiyo itakaa sawa na kupata maendeleo inayoyahitaji kwa watu wake na kupunguza ukali wa maisha.“Ndugu zangu nimesimama hapa kukupeni moyo, nikupeni matumaini kwamba huko tunakoelekea mambo yatakaa sawa na ugumu wa maisha utapungua In shaa Allah” Aliwaahidi wananchi hao.

Aidha, aliwaasa Wazanzibari waendelee kuidumisha amani iliyopo ili wafaidi matunda ya utulivu wa nchi yao kwa kushuhudia zaidi miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ikiwemo afya, maji, elimu na barabara.

Naye, Sheikh Otman Maalim wakati akihutubu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa msikitini hapo, aliwaelezea waumini umuhimu na wajibu wa kutenda mema kwenye mambo ya haki na khairati.Alisema kupeana salam ni moja ya ibada kubwa kwenye na ni haki kupeana kwa uislamu nakuongeza kuwa kuirejesha ni wajibu kwa waamini wanaposalimiwa, aidha alieleza kuitikia mialiko, kuwarehemu wanaopiga chafya,  kuwakagua wagonjwa hospitali pamoja na kulifuata jeneza la muumini aliekufa ni miongoni mwa haki za waumini kufanyiana kwenye mambo ya khairati.Hata hivyo aliwasihi waumini hao kuendelea kupeana nasaha njema na kushauriana kwenye mambo ya kheri yenye kuleta tija kwa manufaa ya taifa.