RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na Taasisi ya JKCI kwa kuanzisha kitengo cha kuhudumia magonjwa ya moyo Zanzibar katika Hospitali ya Mkoa Lumumba.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo wakati akifunga kongamano hilo la Wataalamu wa Kimataifa wa magonjwa ya moyo liloandaliwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI na Wizara ya Afya Zanzibar katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport lililowashirikisha Wataalamu wa Afya ndani na nje ya nchini tarehe: 10 Februari 2024.

Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali kuwekeza katika vifaa vyote vya matibabu ya Moyo Zanzibar.Aidha Rais Dk.Mwinyi ameagiza Wizara ya Afya Zanzibar kuanza haraka majadiliano na Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete JKCI ili huduma za upasuaji wa moyo zianze kutolewa Zanzibar kipindi kifupi kijacho.

Rais Dk. Mwinyi pia amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatenga rasilimali zilizopo ili kuendeleza juhudi za utafiti, kinga na matibabu ya magonjwa ya moyo.Vilevile Rais Dk. Mwinyi amesema dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha huduma za Afya kwa kutoa matibabu ya magonjwa ya moyo na kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amewahimiza wananchi kutumia vyakula vinavyoshauriwa na wataalamu pamoja na kufanya mazoezi.