RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi wa Shehiya ya Kiongwe kuwa Barabara ya Bumbwini - Kiongwe, itajengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika katika kipindi kifupi kijacho.

Dk Mwinyi ametoa ahadi hiyo leo alipozungumza na wananchi wa Shehiya ya Kiongwe na vijiji jirani, baada ya kutembelea na kukaguwa matayarisho ya mradi wa Barabara ya Bumbwini hadi Kiongwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja , sambamba na mradi wa upelekaji umeme na maji safi na salama.

Amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 7.8 inayoanzia Bumbini hadi Kiongwe itajengwa kwa kiwango cha Lami, ambapo matayarisho ya msingi ya ujenzi huo yakiwa yamekamilika.

Rais Dk. Mwinyi alisema kila binadamu anahitaji maji, ikiwa sehemu ya maisha yake, hivyo akaahidi kusimamia uwekaji wa mabomba kwa wastani wa kilomita tano, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana kijijini hapo.

Aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kujenga madarasa sita yanayohitajiwa na wananchi wa shehiya hiyo ili kuwawezesha wanafunzi wa skuli iliopo kijijini hapo kupata huduma za elimu kwa ufanisi.

Aidha,  aliwahakikishia wananchi wa shehiya hiyo kuwa Serikali itatoa unafuu katika kuwaunganishia umeme, huku matayarisho ya kazi hiyo ikiwa katika hatuza za mwisho kukamilika.

Rais Dk. Mwinyi alilitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuhakikisha kijiji jirani na Shehiya hiyo nacho kinapatiwa huduma za umeme ili wananchi wake waweze kunufaika na huduma hiyo.

Dk. Mwinyi alikiri kuwa Wavuvi wa Zanzibar ikiwemo wa kijiji cha Kiongwe wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uvuvi, hivyo kuendelea kutumia vifaa duni na kushindwa kufikia malengo yao na akabainisha mikakati ya serikali katika kuleta mageuzi ndani ya sekta hiyo.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi wa Shehiya ya Donge Chechele kuwa barabara ya Donge Mbiji hadi Chechele yenye urefu wa kilomita mbili itajengwa kwa kiwango cha Lami, pamoja na kulijenga daraja liliopo ili kuwawezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao kutoka mashambani na hivyo kuchochea shughuliza kiuchumi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliweka Jiwe la Msingi la kituo cha Afya Mbuyu Maji pamoja na kutembelea ujenzi wa skuli katika kijiji cha Matemwe Mbuyu Maji, huku akiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufanikisha ujenzi wa madarasa manne ya skuli hiyo ili kukidhi mahitaji ya kielimu.

Vile vile aliliagiza Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kusambaza umeme katika maeneo yote ambayo hayana huduma hiyo kijijini hapo, sambamba na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)kuweka mipango ya mda mfuoi na mrefu ya usambambazaji wa huduma za maji.

Nae, Mwakilishi wa jimbo la Donge Dk. Khalid Salum Mohamed aliwaomba wazazi na walezi wa kijiji cha Chechele kusimamia vyema malezi ya watoto wao ili kuondokana na vitendo viovu, ikiwemo wizi wa mazao pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, huku akibainisha azma ya Serikali ya kuwezesha vijana kiuchumi kuwa haitaweza kufikiwa katika hali hiyo.

Aidha, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mussa Ali Mussa alikiri kuwepo tatizo la wizi wa mazao katika shehiya mbali mbali Mkoani humo ikiwemo Chechele na kubainisha mikakati ya Jeshi hilo katika kupambana na uhalifu.

Kamanda Mussa aliiomba jamii kujenga ushirikiano na Askari Jamii wa Ulinzi shirikishi katika maeneo husika ili kuweza kukabiliana ipasavyo na changamoto hizo za uvunjifu wa sheria.

Nao, baadhi ya wananchi katika maeno mbali mbali walipata fursa ya kuwasilisha changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maeneo yao, ikiwemo ukosefu wa huduma za maji safi na salama, uhaba wa madarasa, uhaba wa wafanyakazi katika vituo vya Afya, vifaa duni vya uvuvi, kushamiri kwa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, na kadhalika.

Mapema, akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Maendeleo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Mei 2021, Mku wa Mkoa huo Ayoub Mohamed Mahamoud alisema Mkoa huo umepata mafanikio makubwa kupitia Programu ya Usambazaji Umeme Vijijini, ambapo jumla ya miradi saba ya umeme imekamilika.

Alisema katika vijiji 109 ambavyo bado havijaunganishwa na Nishati ya umeme, vijiji 57 kati yake vinatarajiwa kuunganishwa na umeme kupitia Bajeti ya mwaka 2021/2022, huku wateja wapatao 10,651 wakitumia nishati hiyo katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii