Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kundi la vijana lina umuhimu mkubwa katika kufanya maamuzi ya Taifa, na ameahidi kuwapatia vijana nafasi zaidi za uongozi katika awamu ijayo.

Dkt. Mwinyi amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutoa kipaumbele kwa vijana katika masuala ya ajira, elimu na fursa za uongozi, akibainisha kuwa Serikali imeongeza bajeti ya elimu kutoka shilingi bilioni 80 hadi bilioni 864, ikiwa ni uthibitisho wa dhamira ya kuhakikisha vijana wote wanaelimika na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Amesema Serikali itaendelea kujenga vyuo vya elimu ya amali katika kila mkoa ili kuwawezesha vijana kupata elimu ya ufundi na stadi za kujiajiri.

Aidha, Dkt. Mwinyi ametangaza mpango wa kuongeza ajira mpya laki 3.5, akiahidi kuvuka lengo hilo kwa kuhakikisha vijana wengi zaidi wananufaika. Ameeleza kuwa maeneo yenye mahitaji makubwa ya ajira ni elimu, afya, vikosi na viwanda, ambapo Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo ya Dunga, Zuze na Pangatupu.

Ameongeza kuwa Serikali itahamasisha ajira kupitia sekta binafsi na kuongeza mikopo kwa vijana ili waweze kujiajiri wenyewe, sambamba na kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Akizungumza katika mkutano na makundi mbalimbali ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ikiwemo kutoka vyuo na vyuo vikuu uliofanyika katika Chuo cha Vijana wa CCM, Tunguu, Dkt. Mwinyi amesema katika awamu ijayo atawateua vijana wengi zaidi kushikakushika nafasi za uongozi, akisisitiza kuwa “Wakati huu ni wa vijana kwa sababu wana elimu, uwezo na ari ya kuijenga Zanzibar.”

Vilevile, ameahidi kujenga miundombinu imara kwa jumuiya za CCM, ikiwemo ofisi na kumbi za mikutano, ili kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi.Akijibu hoja za vijana, Dkt. Mwinyi ameahidi kuongeza posho kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika awamu ijayo kutokana na ongezeko la mahitaji na changamoto wanazokabiliana nazo.

Kwa kuunga mkono jitihada za ubunifu, ameeleza kuwa Serikali itaanzisha Wizara Mpya ya Mawasiliano na Ubunifu katika awamu ijayo, ili kuendeleza miradi ya ubunifu inayoanzishwa vyuoni na kuijengea Taifa uchumi wa kisasa.Akiwataka vijana kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, Dkt. Mwinyi amewasihi kumchagua tena ili aweze kutekeleza ahadi zote anazozitoa kwa vitendo.